LIVE STREAM ADS

Header Ads

Shirika la AGPAHI latoa mafunzo kwa akina mama rika mkoani Mwanza

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com

 Shirika la Ariel Glaser Pediatric AIDS Healthcare Initiative (AGPAHI) linayojihusisha na mapambano dhidi ya VVU/ Ukimwi limetoa mafunzo ya siku mbili kuanzia leo Aprili 24, 2019 kwa akina mama rika kutoka Wilaya za Mkoa Mwanza kwa ajili ya kuwajengea uwezo ili kusaidia mapambano dhidi ya ugonjwa huo katika jamii.

Shirika hilo kwa ufadhili wa Watu wa Marekani kupitia taasisi ya Centres for Disease Control (CDC), limekuwa likishirikiana na Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kutekeleza afua mbalimbali za kupambana na maambukizi ya VVU/ Ukimwi pamoja na kuwahudumia wanaoishi na maambukizi hayo.
Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
 Mwezeshaji wa mafunzo hayo kutoka mkoani Pwani, Dkt. Happness Mbeyela akiwasilisha mada kuhusu masuala ya VVU/Ukimwi na watoto kwenye mafunzo hayo.
 Mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo akina mamarika mkoani Mwanza kuzingatia ufuasi mzuri wa dawa za VVU pamoja na kutoa elimu kupambana na maambukizi hayo kwa wengine.
 Mwezeshaji wa mafunzo hayo kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga, Dkt. Edwiga Zumba akiwasilisha mada kuhusu ufuasi mzuri wa dawa kwenye mafunzo hayo.
 Mmoja wa wawezeshaji wa mafunzo hayo, Yahaya Isangula ambaye ni Muuguzi kutoka Hospitali ya Wilaya Misungwi akifafanua jambo kwenye mafunzo hayo.
 Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo kutoka Wilaya za Mkoa Mwanza akichangia mada.
Mshiriki Amina Khamis kutoka Kituo cha Afya Igoma jijini Mwanza akichangia mada kwenye mafunzo hayo.
 Shirika la Ariel Glaser Pediatric AIDS Healthcare Initiative (AGPAHI) kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania pamoja na wadau mbalimbali kwa ufadhili wa Watu wa Marekani kupitia taasisi ya Centres for Disease Control (CDC) limekuwa likiendesha afua mbalimbali kupambana na maambukizi ya VVU/ Ukimwi.
 Washiriki wakifuatilia mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Shirika la Ariel Glaser Pediatric AIDS Healthcare Initiative (AGPAHI).
 Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo kutoka Wilaya za Mkoa Mwanza ambazo ni Nyamagana, Ilemela, Sengerema, Misungwi na Magu.
 Baadhi ya wanahabari walioshiriki mafunzo hayo.
 Tazama BMG Online TV hapa chini

Na Kadama Malunde, Malunde 1 Blog
Ariel Glaser Pediatric AIDS Healthcare Initiative (AGPAHI) ambayo ni asasi ya kitaifa isiyo ya kiserikali inayojihusisha na mapambano dhidi ya Virusi Vya UKIMWI na UKIMWI imeendesha warsha kwa MAMA RIKA mkoa wa Mwanza ili kuwajengea uwezo kuhusu masuala mbalimbali ya Virusi vya UKIMWI (VVU) na UKIMWI.

MAMA RIKA ni Waelimishaji wa akina mama wajawazito na wanaonyonyesha wenye maambukizi ya VVU ambao wanapata huduma za tiba na matunzo katika kliniki za kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto (PMTCT).

Warsha hiyo ya siku mbili iliyoanza Aprili 24,2019 inafanyika katika ukumbi wa Gold Crest Hoteli Jijini Mwanza na kukutanisha pamoja MAMA RIKA 70 kutoka halmashauri za wilaya mkoa wa Mwanza.

Mwezeshaji wa Kitaifa wa Masuala ya Vijana, VVU na UKIMWI, Dk. Happiness Wimile Mbeyela alisema lengo la warsha hiyo ni kuwajengea uwezo kuhusu masuala ya VVU na UKIMWI hususani uzuiaji wa maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.

“Tupo hapa kwa ajili ya kuwajengea uwezo akina mama wanaoishi na VVU kuhusu masuala ya VVU na UKIMWI ili wakatoe elimu kwa akina mama wengine ili wafike kwenye vituo vya afya wanapokuwa wajawazito”,alisema Dk. Mbeyela.

“Tunawapa ujuzi wa kupigana na unyanyapaa,umuhimu wa kujiweka wazi,jinsi ya kunyonyesha na kuwa wafuasi wazuri wa dawa za kupunguza makali ya VVU (ARVs)
,akina mama hawa watakwenda kutoa elimu kwa akina mama wengine na kuwasisitiza wajiunge kwenye vikundi”,aliongeza Dk. Mbeyela.

Kwa upande wake,Mwezeshaji katika warsha hiyo, Edwiga Zumba alitoa wito kwa akina mama wajawazito kufika kwenye vituo vya afya na wanapobainika kuwa na maambukizi ya VVU waanze tiba kwa ajili ya kuwakinga watoto wasipate maambukizi ya VVU.

“Akina mama hudhurieni kliniki,nendeni mkajifungulie hospitali,huko kuna wataalamu wa afya waliobobea ili kupunguza idadi ya watoto wanaozaliwa na VVU kwani maambukizi hutokea wakati wa ujauzito,kujifungua na wakati wa kunyonyesha”,alisema Zumba.

Nao washiriki wa warsha hiyo,walisema bado kuna changamoto ya baadhi ya akina mama kutokubali kuwa wana maambukizi ya VVU licha ya vipimo kuonyesha kuwa wamepata maambukizi.

“Tukubaliane na hali,kama umeonekana una maambukizi ya VVU,anza kutumia dawa za ARVs na endelea kupima badala ya kuacha kutumia dawa kwani ukipuuzia utajikuta unazaa mtoto mwenye maambukizi matokeo yake mtoto huyo atakulalamikia kuwa ulimwambukiza kwa maksudi”,alieleza Amina Khamis kituo cha afya Igoma.

No comments:

Powered by Blogger.