Wadau waadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika 2019 mkoani Shinyanga
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Na Marco Maduhu, Malunde1 Blog
Mashirika ya KIWOHEDE na AGAPE ACP ambayo yanatekeleza miradi ya kupinga matukio ya ukatili dhidi ya watoto wadogo na kutokomeza mimba na ndoa za utotoni mkoani Shinyanga yameungana pamoja kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika.
Siku ya Mtoto wa Afrika hufanyika kila mwaka Juni 16 ambapo mwaka huu 2019 kwa Mkoa Shinyanga yamefanyika kwenye uwanja wa michezo wa Taifa wilayani Kahama, mgeni rasmi akiwa Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Anamringi Macha aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa Shinyanga, Zainab Telack.
Macha aliitaka jamii kuachana na vitendo vya ukatili dhidi ya watoto ambapo aliwasisitiza wazazi kuacha tabia ya kuwafanyia vitendo vya kikatili watoto wao pamoja na kuwabagua kuwapatia elimu na kufikia hatua ya kuwaozesha ndoa za utotoni wanafunzi wa kike.
Alisema serikali haitasita kuchukua hatua za kisheria kwa yeyote atakayekamatwa akiwafanyia ukatili watoto huku akitumia fursa hiyo kuyapongeza mashirika yasiyo ya kiserikali mkoani humo ikiwemo KIWOHEDE na AGAPE kwa kazi nzuri ambayo yamekuwa yakiifanya ya kushirikiana na Serikali kutatua changamoto mbalimbali ndani ya jamii.
Naye Mratibu wa Mradi wa Elimu ya Afya ya Uzazi, Jinsia na Haki kwa Vijana wa Shirika la KIWOHEDE, Amos Juma aliitaka jamii kuachana na vitendo vya kunyanyasa watoto wao pamoja na kuacha tabia ya kuendekeza mila na desturi kandamizi kwa kuwaozesha watoto na hatimaye kuzima ndoto zao.
Alisema katika mradi wao wa elimu ya afya ya uzazi na ujinsia na kutetea haki za vijana, ambao wanautekeleza kwenye kata ya Zongomela, wamekuwa wakikumbana na changamoto ya jamii kupenda kuendekeza mila na desturi zilizopitwa na wakati, na hivyo kuwapatia changamoto kubwa ya kumaliza kabisa ukatili kwa watoto licha ya kuupunguza kwa asilimia kubwa.
"KIWOHDE kama wadau wakubwa wa kutetea haki za watoto, tunapenda kutumia fursa hii kwenye maadhimisho haya ya siku ya mtoto wa Afrika Duniani, kuwataka wazazi waachane na mila kandamizi pamoja na kuwafanyia vitendo vya ukatili watoto wao, bali wawatekelezee mahitaji hayo pamoja na kuwapatia elimu bila ya kuwabagua ili wapate kutimiza ndoto zao" alisema Juma na kuongeza;
"Mradi huu tulianza kuutekeleza mwaka 2017 na unatarajiwa kuisha mwaka huu 2019 ambapo kipindi tunauanza kuutekeleza kwenye Kata ya Zongomela, kulikuwa na matukio mengi ya ukatili dhidi ya watoto zikiwamo na mimba za wanafunzi, lakini kwa sasa matukio hayo yamepungua kwa kiasi kikubwa tofauti na awali" alibainisha.
Kwa upande wake Msimamizi wa Mradi wa Sauti ya Mwanamke na Mtoto kutoka Shirika la AGAPE mkoani Shinyanga, Felix Ngaiza alitoa raai kwa jamii kuachana na vitendo vya ukatili pamoja na ndoa za utotoni.
Ngaiza alisema Shirika la AGAPE litaendelea kushirikiana na Serikali na jamii ili kuhakikisha watoto na wanawake wanapata haki kwa wakati. Kauli mbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika 2019 ni "Mtoto ni Msingi wa Taifa Endelevu, Tumtunze, Tumlinde na Kumwendeleza".
No comments: