LIVE STREAM ADS

Header Ads

Tume ya kurekebisha Sheria yakabidhi ripoti ya mapendekezo Sheria ya Ufilisi

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com

Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Dkt. Augustine Mahiga (kulia) akimkabidhi Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya RITA Profesa Hamisi Dihenga (kushoto) ripoti ya mapendekezo ya marekebisho ya sheria ya Ufilisi baada ya kukabidhiwa kutoka kwa Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria, zoezi hilo limefanyika jijini Dodoma.

Wanaoshuhudia ni Katibu Mkuu Wizara Wizara ya Sheria na Katiba, Profesa Sifuni Mchome (wa tatu kulia) na Kaimu Kabidhi Wasii Mkuu wa RITA, Emmy Hudson (wa pili kulia).
#BMGHabari
Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Dkt. Augustine Mahiga (kushoto) akikabidhiwa ripoti kuhusu mapendekezo ya marekebisho ya sheria ya Ufilisi.
Kikao cha uzinduzi wa bodi.

Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Dkt. Augustine Mahiga amepokea ripoti ya mapendekezo ya sheria yaliyowasilishwa jana na Tume ya Kurekebisha Sheria jijini jini Dodoma.

Akipokea taarifa hiyo, Balozi Dkt. Augustine Mahiga alifurahishwa kwa kazi nzuri iliyofanywa na Tume hiyo pamoja na wadau mbalimbali waliofanikisha kukamilika kwa mapendekezo ya sheria ya Ufilisi na nyingine zilizowasilishwa katika tume hiyo ambazo ni sheria ya Ushahidi na ile ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.

"Nimeridhishwa kwa kazi nzuri iliyofanyika kwani tunakwenda kupata sheria madhubuti itakayoendana na hali ya sasa na kusimamia kikamilifu misingi ya utawala bora" alisema Balozi Dkt. Mahiga.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria, Januari Msofe alisema kuwa tume yake imefanya mapitio na utafiti wa kina kuhusu mifumo ya Sheria zinazosimamia Ufilisi na kubaini mapungufu ya kisheria na kiutendaji ambao umeathili utekelezaji wa masuala ya hayo hapa Nchini.

Alibainisha mapungufu hayo ni pamoja na kuwepo kwa sheria mbalimbali za kisekta kama vile sheria ya Makampuni sura ya 212, sheria ya mabenki na taasisi za kifedha sura ya 342, sheria ya vyama vya ushirika sura ya 211, Sheria ya bima sura ya 394, sheria ya mashirika ya umma Sura ya 57 na sheria ya usajili wa wadhamini sura ya 318 na hivyo kukosekana kwa sheria mahsusi inayosimamia jukumu la ufilisi pekee na kusababisha mkanganyiko kwa watumiaji kufanya maamuzi ya sheria ipi inaweza kutatua matatizo yanayowakabili.

Hata hivyo kuwepo kwa sheria hizo kumesababisha matatizo kwa wadai kutojua taratibu za kupata haki zao kwa wakati pamoja na kuwepo kwa taratibu ndefu zinazochelewesha mashauri ya ufilisi kumalizika kwa wakati mara baada ya taasisi au kampuni husika kufilisika.

Aliongeza kuwa Sheria zinazotumika hivi sasa zimepitwa na wakati ambazo baadhi yake zinatoa adhabu na faini ndogo kwa wale wanaokiuka taratibu za ufilisi kwa mfano faini ya shilingi 200 kiasi ambacho hakiendani na kiwango cha uchumi na maisha ya sasa huku zikitambua njia moja tu ya mawasiliano ambayo ni posta pekee huku ikiacha nyuma maendeleo makubwa upande wa teknolojia ya habari na mawasiliano.

Vilevile ugumu wa taratibu za kisheria katika ufilisi wa makampuni ya nje yenye kampuni tanzu Tanzania na hivyo kuziachia kampuni hizo kutumia sheria za nchi zao na kusababisha tatizo la kiuchumi katika nchi yetu kutokana na sheria zetu kukosa nguvu ya kuyadhibiti makampuni hayo tofauti na nchi jirani ya Kenya na Uganda ambazo zimeweka sheria na taratibu nzuri za kufuata kwa makampuni ya nje yenye kampuni tanzu kwenye nchi zao.

Mapungufu ya sheria hizo pia kumesababisha kuwepo kwa mamlaka na vyombo mbalimbali vinavyosimamia masuala ya ufilisi kama vile kuangalia mali za kampuni pale inapofikia hatua ya kufilisika na mahakama kuteua chombo au taasisi yoyote inayoshughulika na ufilisi badala ya Taasisi ya RITA ambayo kisheria ndiyo yenye mamlaka kisheria ya kuwa msimamizi na mratibu wa masuala yote ya ufilisi.

Hafla ya kukabidhi ripoti hiyo ilihudhuriwa na baadhi ya Wakuu wa Taasisi, Watumishi wa Wizara ya Katiba na Sheria, Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), Ofisi ya Mwanasheria Mkuu pamoja Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

No comments:

Powered by Blogger.