LIVE STREAM ADS

Header Ads

Vyama vya wagiliaji vyatakiwa kuwa na usimamizi thabiti wa skimu za umwagiliaji

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Mkurugenzi wa Idara ya Mafunzo na Utafiti kutoka Wizara ya Kilimo, Wilhelm Mafuru akifungua kongamano la mashindano ya vyama vya umwagiliaji kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mhandisi Mathew Mtigumwe hii leo jijini Dodoma.
Washiriki wakifuatilia kongamano hilo la mashindano ya vyama wa umwagiliaji.
Katibu Mkuu Mstaafu Wizara ya Kilimo, Mhandisi Mbogo Mfutakamba akifafanua jambo kwa waandishi wa habari kuhusiana na umuhimu wa kilimo cha umwagiliaji na Tanzania ya viwanda.
Frida Tarimo ambaye ni mkulima wa zao la mpunga katika skimu ya kilimo cha umwagiliaji Simanjiro akieleza manufaa ya mafunzo ya utunzaji na uendeshaji wa miundombinu ya umwagiliaji katika kongamano hilo.
Washiriki wa kongamano la mashindano ya vyama vya umwagiliaji lililofanyika jijini Dodoma wakiwa kwenye picha ya pamoja.

Mwandishi Maalum, Dodoma
Wakulima wa kilimo cha umwagiliaji nchini kupitia skimu za umwagiliaji, wametakiwa kuwa na usimamizi thabiti wa skimu hizo ili kilimo hicho kuwa cha uhakika zaidi na chenye tija kwa mkulima na taifa kwa ujumla.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe, Mkurugenzi wa Idara ya Mafunzo na Utafiti katika Wizara hiyo, Wilhelm Mafuru ameyasema hayo leo jijini Dodoma kwenye kongamano la mashindano ya vyama vya umwagiliaji nchini.

Kongamano hilo limeshirikisha vyama 36 na kushindanisha vyama vinane vya umwagliaji kutoka Kanda nane za umwagiliaji likiwa na lengo la kutoa motisha kwa skimu zilizowahi kupata mafunzo ya matunzo na uendeshaji chini ya mradi wa kujenga uwezo kwa wataalamu wa umwagiliaji wa TANCAID awamu ya pili kupitia shirika la kimataifa la maendeleo la Japan JICA kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji. 

Kadhalika warsha imetoa fursa kwa wadau wa umwagiliaji kuona namna ya kuendeleza miundombinu ya umwagiliaji, pamoja na kutoa nafasi kwa vyama vya umwagiliaji kubadilishana uzoefu wa namna bora yakuendesha na kutunza skimuza umwagiliaji.

Mafuru amesema Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imeendelea kusaidia wakulima kupata elimu kupitia wataalam ili kuweza kulima kwa tija na kuendelea kusimamia na kuimarisha shughuli za kilimo cha umwagiliaji.

Akiongea kwa Niaba ya wakulima wa skimu ya umwagiliaji ya Lemkuna, mkulima FridaTarimo amesema kupitia mafunzo wanayopata, wameweza kusimamia uendeshaji na matunzo ya miundombinu ya umwagiliaji, upatikanaji wa maji ya kutosha kwenye vitalu na maandalizi mazuri ya kalenda ya msimu wa kilimo jambo ambalo ameeleza kwamba limeongeza uzalishaji katika kilimo hususani katika zao la mpunga.

Awali akiongea na waandishi wa habari, Katibu Mkuu Mstaafu, Wizara ya Kilimo, Mhandisi Mbogo Futakamba amebainisha kwamba kilimo cha umwagiliji kinahitaji uwekezaji mkubwa, miundombinu bora na mfumo sahihi wa umwagiliaji jambo ambalo linaweza kuleta uhakika wa chakula na malighafi kwa ajili ya viwanda na hivyo dhana ya Tanzania ya Viwanda kufikiwa.

No comments:

Powered by Blogger.