LIVE STREAM ADS

Header Ads

Serikali ya Austria yaunga mkono maendeleo mkoani Singida

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida Vijijini, Mwl. Omari Kachebele (katikati) akikata utepe kuashiria upokeaji wa madarasa madarasa mawili na ofisi ya walimu yaliyokarabatiwa na Shirika lisilokuwa la kiserikali la Community Initiatives Promotion (CIP) katika hafla iliyofanyika katika Shule ya Msingi Ikhanoda iliyopo Ilongero mkoani Singida. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la CIP, Afesso Ogonga.
Mwonekano wa madarasa hayo baada ya kukarabatiwa.
Viongozi mbalimbali wakiwa kwenye picha ya pamoja na wanafunzi.
Wanafunzi wakiimba nyimbo kufurahia kukabidhiwa madarasa hayo. 
Wananchi wakiwa kwenye mkutano wa hadhara.
Mkurugenzi Mtendaji wa CIP, Afesso Ogonga akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara.
Mkurugenzi Mtendaji wa CIP, Afesso Ogonga akikabidhi vifaa tiba kwa mgeni rasmi, Mwl. Omari Kachebele.

Na Dotto Mwaibale, Singida
Serikali ya Austria kupitia shirika la Sister Cities Salzburg- Singida (SCSS) lililoko Salzburg Austria kwa kushirikiana na shirika lisilokuwa la kiserikali la Community Initiatives Promotion (CIP) la mkoani Singida, imeunga mkono jitihada za Rais Dkt. John Magufuli katika kuinua sekta za elimu na afya nchini kupitia miradi mbalimbali inayofadhiliwa ambapo limekarabati madarasa mawili na ofisi ya walimu katika Shule ya Msingi Ikhanoda iliyopo Halmashauri ya Wilaya Singida Vijijini. 

Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la CIP, Afesso Ogenga akikabidhi madarasa hayo alisema Ushirikiano wa maendeleo wa mashirika hayo ulianza tangu miaka 1980 ambapo miradi mingi imetekelezwa na kuchangia maendeleo kwa kiasi kikubwa ndani ya mkoa wa Singida. 

Alisema katika mwaka wa fedha 2018-2019, SCSS limetoa takribani sh. 135 milioni fedha za kitanzania kusaidia miradi ya maendeleo katika kata za Mwasauya na Ikhanoda zilizopo katika halmashauri hiyo. 

"Fedha hizo zimetumika katika kutekeleza miradi katika sekta ya Elimu- ujenzi wa madarasa mawili na ofisi moja ya waalimu katika shule ya msingi ya Ikhanoda, mafunzo kwa waalimu wa hisabati na kiingereza toka kata za Ikhanoda na Mwasauya" alisema Ogenga.

Aliongeza kuwa katika sekta ya afya shirika limejikita katika kupunguza vifo vya wakina mama wajawazito na watoto wa chini ya umri wa miaka mitano kwa kutoa mafunzo kwa wauguzi na wakunga (Refresher training in maternal and new born health to nurses and midwives) na mafunzo ya muda mrefu (Diploma/degree scholarship), kuwajengea uwezo wahudumu wa afya katika ngazi ya jamii (Community health workers), kuelimisha jamii na kusaidia uanzishwaji wa bustani za nyumbani (kitchen garden) kwa lengo la kuimarisha lishe kwa watoto.

Alisema shirika limeweza kutoa vifaa tiba katika zahanati nne za Ikhanoda, Kisisi, Mdilu na Ngamu katika kata za Ikhanoda na Mwasauya na kuwa katika sekta ya maendeleo ya jamii, shirika limejikita kuwasaidia wanawake kuongeza kipato kupitia miradi ya ufugaji wa kuku kwa njia za kisasa ambapo Wakina mama wapatao 60 wamepatiwa mafunzo, na kupewa vifaa mbalimbali kama vile waya wa uzio, vifaa vya kulishia na kunyweshea kuku, vifaranga na huduma ya chanjo.

Akizungumza katika hafla ya kukabidhiwa madarasa hayo iliyofanyika mwishoni mwa wiki katika shule ya msingi Ikhanoda , Mwenyekiti wa Kijiji cha Ikhanoda, Jumanne Idabu alisema shirika hilo limekarabati madarasa hayo kwa kupiga lipu, kuweka sakafu, kuweka madirisha 12 yenye shata za vioo, milango mitatu, kupaka rangi kuta, mbao na mabati na kuchangia gharama za ufundi.

Mgeni rasmi wa makabidhiano hayo, Mwl. Omari Kachebele akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo alilishukuru shirika hilo na wafadhili SCSS kwa shughuli za maendeleo ya wananchi linazozifanya katika kata hiyo tangu lianze kufanya kazi june mwaka jana.

Pia Mratibu wa Miradi wa Shirika hilo, Violet Shaku aliwashukuru viongozi wa vijiji, wakazi na watumishi wa serikali katika kata za Ikhanoda na Mwasauya kwa ushirikiano walioonyesha wakati wa kutekeleza miradi hiyo. Aliongeza kuwa shirika litaendelea kusaidia kuinua zaidi elimu na afya katika mwaka wa fedha wa 2019/20 katika Wilaya ya Singida vijijini.

Mkazi wa Kata hiyo Gabriel Nkumbi (74) alilishukuru shirika hilo kwa msaada huo na kuwa kama litapata fursa nyingine liwapelekee miradi mingine kwa sababu mahitaji bado ni mengi. Aidha alisema jamii iko tayari kushirikiana na shirika hili katika miradi mingine. Alionyesha kuvutiwa na namna shirika linavoshirikisha jamii kuanzia hatua za awali za mradi mpaka mwisho.

Elizabeth Hinga akizungumza kwa niaba ya wanawake wa Kata hiyo alisema wanalishukuru shirika hilo kwa kuwapelekea vifaa tiba kwa ajili ya kuwasaidia wakati wakijifungua zikiwemo mashine ya kupima mapigo ya moyo ya mtoto aliyezaliwa, kupima kiwango cha damu, vifaa vya kujifungua (delivery and evacuating kit) na mizani za kupimia uzito.

No comments:

Powered by Blogger.