LIVE STREAM ADS

Header Ads

Mchakato ujenzi wa Taasisi ya Moyo Kanda ya Ziwa waanza

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Judith Ferdinand, BMG
Hospitali ya Rufaa Kanda ya Ziwa Bugando kwa kushirikiana na Serikali ngazi ya Mkoa Mwanza, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeanza mchakato wa ujenzi wa taasisi ya moyo ili kusogeza karibu upatikanaji wa huduma kwa wananchi.

Ujenzi huo utakao gharimu takribani bilioni 59 utasaidia wananchi kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa kupata matibabu yanayohusiana na ugonjwa wa moyo kwa urahisi huku wakiokoa muda na gharama za kusafiri hadi jijini Dar es salaam ama nchi jirani kusaka huduma hiyo.

Mkurugenzi wa Hospitali ya Bugando Profesa, Abel Makubi aliyasema hayo Septemba 05, 2019 wakati akitoa taarifa ya maboresho ambayo yamefanyika katika idara mbalimbali za hospitali hiyo kwa Maafisa Habari, Mawasiliano na Mahusiano kwa Umma kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Hospitali pamoja na Taasisi zilizo chini ya wizara hiyo ambao walitembelea hospitalini hapo.

Profesa Makubi alisema hatua hiyo imekuja baada ya kubainika kwamba takribani asilimia 30 hadi 40 ya wagonjwa wanaopata matibabu katika taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete jijini Dar es salaam hutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa.

"Sisi hospitali ya Bugando kwa kushirikiana na Serikali yetu ya Mkoa Mwanza pamoja na Wizara ya Afya tumeanza mchakato wa ujenzi wa taasisi ya moyo karibu na Hospitali yetu ambapo hadi kukamilika itagharimu fedha za kitanzania takribani bilioni 59" alisema Profesa Makubi.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma Hospitali ya Taifa Muhimbili, Aminiel Aligaesha alisema Bugando ni Hospitali ya pili kwa ukubwa hivyo maboresho hayo yatasaidia kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi ambapo inakadidiriwa takribani wagonjwa elfu kumi na tano wanahudumiwa hospitalini hapo kwa siku kama iliyo Muhimbili.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali kutoka Wizara ya Afya, Gerald Chami alisema lengo la ziara hiyo ni kujifunza na kujengeana uwezo katika kutangaza maboresho yaliyofanywa na Serikali katika kuboresha sekta ya afya pamoja na kujionea mafanikio yaliyopatikana katika hospitali ya Bugando.
Tazama BMG Online TV hapa chini

No comments:

Powered by Blogger.