LIVE STREAM ADS

Header Ads

Bugando Mpya "Muhimbili wafurahia maboresho yaliyofanyika Bugando"

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Judith Ferdinand, BMG
Uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Ziwa Bugando kwa kushirikiana na Serikali, umefanikiwa kufanya maboresho katika idara mbalimbali za hospitali hiyo ikiwemo upatikanaji wa huduma ya CT-Scan na maabara.

Mkurugenzi wa Hospitali hiyo, Profesa Abel Makubi aliyasema hayo Septemba 05, 2019 wakati akizungumza na Maafisa Habari, Mawasiliano na Mahusiano kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto, Hospitali na taasisi mbalimbali zilizo chini ya wizara hiyo waliofanya ziara ya kutembelea hospitalini hapo.

"Kwa kipindi cha miaka minne cha uongozi Serikali ya awamu ya tano kwa kushirikiana na Hospitali ya Bugando, tumefanikiwa kuboresha hospitali yetu katika maeneo mbalimbali ikiwemo huduma za CT-Scan, maabara, ujenzi wa maabara ya uchunguzi wa vinasaba, uimarishaji wa uchunguzi wa magonjwa ya mfumo wa chakula na tumbo" alisema Profesa Makubi na kuongeza;

"Tumeanzisha tiba ya Saratani kwa Kanda hii ya Ziwa ambapo wizara imejenga jengo lenye thamani ya bilioni 5.5, uboreshaji wa huduma za dharura Kanda ya Ziwa, upanuzi na uboreshwaji wa kitengo cha kusafisha figo, upanuzi na ujenzi wa vyumba vya upasuaji, uanzishwaji wa kliniki mpya za kibingwa, uanzishwaji wa kliniki ya wagonjwa wa bima na mikataba, utoaji huduma kwa mfumo wa kieletroniki, mafunzo ya huduma bora na uboreshaji wa upatikanaji wa dawa ndani ya hospitali," alibainisha.

Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Dharura na Ajali Hospitali ya Bugando, Dkt. Erasto Sylvanus alisema hospitali imefanya ukarabati na upanuzi wa idara hiyo katika maeneo tofauti ikiwemo kuweka mitambo ya kisasa ya huduma ya dharura, dawa, vifaa na mashine ya kupumulia, wodi ndogo ya wagonjwa mahututi (ICU) ambayo wanaitumia kabla ya kumpeleka mgonjwa ICU kubwa.

Alisema pia umefanyika ukarabati vyumba viwili vya upasuaji katika idara hiyo ambapo wanaweza kuwafanyia upasuaji watu wawili kwa wakati mmoja na kuongeza vitanda vya wagonjwa kutoka 14 vya awali hadi 24 hivyo wodi ina uwezo wa kuhudumia wagonjwa 100 kwa wakati mmoja tofauti na 50 wa awali.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma Hospitali ya Taifa Muhimbili, Aminiel Aligaesha alisema Bugando ni hospitali ya pili kwa ukubwa nchini hivyo ina mzigo mkubwa wa kuhudumia wananchi wa Kanda ya Ziwa ambapo inakadiriwa kwa siku inahudumia zaidi ya wagonjwa elfu 10 kama ilivyo Muhimbili.
"Katika ziara hii tumeshuhudia maboresho yaliyofanywa na hospitali ya Bugando kwa kushirikiana na Serikali katika vitengo mbalimbali ambapo nimefurahishwa na upatikana wa dawa" alisema Aligaesha.
Tazama BMG Online TV hapa chini

No comments:

Powered by Blogger.