LIVE STREAM ADS

Header Ads

Wakazi wa Ikungi mkoani Singida wapigwa msasa kupinga Ukeketaji

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Wakazi wa Kata ya Iseke, wanafunzi kutoka Shule za Ihanja, Unyangwe na Nkhoiree pamoja na Maafisa wanaosimamia mradi wa kupambana na mila potofu ya ukeketaji na ukatili wa kijinsia wakionesha mshikamano wa kutokomeza kabisa vitendo hivyo katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Iseke Wilaya Ikungi mkoani Singida.
Mratibu wa mradi wa kupambana na mila potofu ya ukeketaji, Evaline Lyimo akizungumza na wanafunzi wakati wa kuimarisha klabu za watoto mashuleni za kupinga ukatili wa kijinsia na ukeketaji.
Afisa Maendeleo ya Jamii Kata ya Muhintiri, Anatory Mzuma akizungumza na wanafunzi hao.
Wanafunzi wa Shule ya Msingi Unyangwe wakitoa burudani ya ngoma ya asili ya kabila la Wanyaturu.
Picha ya pamoja baada ya kuimarisha klabu za wanafunzi.
Mratibu wa mradi huo, Evaline Lyimo akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Iseke.
Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa watoto na akina mama Kata ya Iseke wakitambulishwa kwenye mkutano huo.
Mwezeshaji wa mradi, Japhet Kalegeya akizungumza kwenye mkutano huo.
Wananchi wakifuatilia kwa umakini mkutano huo.
Mzee Emmanuel Lie (89) akizungumza kwenye mkutano huo.
Mzee Edward Migamba (68) akizungumza.
Mama Eliwanje Ibrahim akizungumza.
Mama Maria Jason akichangia jambo katika mkutano huo.
Mwanafunzi Prisca Elifaraja akielezea changamoto zinazochangia wanafunzi kupata mimba.
Wananchi wakiangalia sinema ya mafundisho namna ya kujikinga na vishawishi kwa wanafunzi kupata mimba.

Na Dotto Mwaibale, Singida
Zaidi ya wananchi elfu kumi (10,258) katika Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi mkoani Singida wamepatiwa elimu ya kutokomeza ukatili wa kijinsia na ukeketaji kwa wanawake na watoto.

Hayo yameelezwa na Mratibu wa mradi wa kupambana na mila potofu ya ukeketaji wilayani humo, Evaline Lyimo katika mkutano wa hadhara wa uhamasishaji wa utetezi dhidi ya mila potofu kama ukeketaji wanawake na wasichana na udhalilishaji wa kijinsia uliofanyika Kata ya Iseke.

"Tumefanikiwa kutoa elimu ya kutokomeza ukatili huo katika Kata tatu za Ihanja, Ikungi na Iseke ambapo jumla ya watu 10,258 wanaume wakiwa 1200, wanawake 2400 na wale wasio wa moja kwa moja wakiwa ni 6,658 tuliwafikia kwa kufadhiliwa shilingi milioni 40 na Shirika la Foundation for Civil Society (FCS)" alisema Lyimo.

Akizungumza katika mkutano huo ulioenda sanjari na kampeni ya kuimarisha klabu za watoto wa shule za msingi na sekondari za kupinga ukatili huo, Mwezeshaji wa mradi huo Japhet Kalegeya alisema mikutano na kampeni hizo zinasaidia kutoa elimu ya kutokomeza kabisa vitendo hivyo ambavyo vipo kinyume na haki za binadamu.

Mzee Emanuel Lie (89) alisema baadhi ya mambo yanayochangia udhalilishaji na mimba kwa wanafunzi ni wazazi na walezi kushindwa kusimamia malezi ya watoto wao.

Mkazi mwingine wa kata hiyo, Edward Migamba (68) alisema umbali mrefu kutoka kijijini na zilipo shule unachangia watoto kupata mimba ambapo mama Eliwanje Ibrahim aliongeza kuwa utandawazi nao ni sababu nyingine ya janga hilo.

Mwanafunzi wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Unyangwe, Prisca Elifaraja akizungumza kwa niaba ya wenzake alisema kutembea umbali mrefu porini wakati wa kwenda shuleni, kukosa chakula na wazazi wanapotoa adhabu ya kuwafukuza watoto nyumbani pale wanapokuwa wamefanya makosa huchangia watoto kujikuta wakiangukia katika vishawishi na kupata mimba na kubakwa.

Mkutano na kampeni za kuimarisha klabu hizo za watoto mashuleni uliandaliwa na Shirika lisilo la Kiserikali la Save the Mother and the Children of Central Tanzania (SMCCT) na kuhudhuria na wanafunzi kutoka Shule za Ihanja, Unyangwe na Nkhoiree ulihitishwa na sinema ya kutoa mafunzo ya kuepuka vitendo vinavyoweza kuwashawishi wanafunzi kupata mimba.

No comments:

Powered by Blogger.