Wahitimu Chuo cha VETA 2019 mkoani Shinyanga wapewa mbinu
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Mahafali hayo yalifanyika Novemba 15, 2019 kwenye viwanja vya chuo hicho huku mgeni rasmi akiwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Shinyanga Mjini (SHUWASA) Flaviana Kifizi.
Akizungumza kwenye Mahafali hayo, Kifizi aliwataka wahitimu hao kujiunga kwenye vikundi vya ujasiriamali ili waweze kupata fedha za Halmashauri za mapato ya ndani asilimia 10 ambazo hutolewa kwa vijana asilimia nne ili wapate mitaji na kujiajiri wenyewe kuliko kupoteza ujuzi wao kwa kusubiri kuajiriwa na kuanza kulalamika maisha magumu.
"Natoa wito kwa wahitimu wa fani mbalimbali ambao mnahitimu leo muache tabia ya kutegemea kuajiriwa, bali mjijenge kujiajiri wenyewe kwani ujuzi mnao,muutumie kujipatia kipato na kuinuka kiuchumi" alisema Kifizi na kuongeza;
"Pia mjiunge kwenye vikundi vya ujasiriamali ili mpate mitaji na kufungua ofisi zenu na kujiajiri wenyewe kuliko kumaliza masomo yenu hapa na kuishia kukaa mitaani na kulalamika hakuna ajira na wakati ujuzi mnao" alibainisha Kifizi.
Katika hatua nyingine aliwataka wafanyabiashara kuchangamkia fursa ya kujenga hosteli jirani na chuo hicho cha Veta ili kuondoa changamoto ya wanafunzi kupanga kwenye magheto na kuangukia kwenye hatari ya kupata ujauzito kabla ya wakati pamoja na wengine kuwa watoro sugu na kuacha masomo.
Akisoma risala kwa niaba ya wahitimu wenzake, Magreth Edward alisema changamoto kubwa ambayo hukabiliana nayo ni ukosefu wa ajira huku wakiomba Serikali kulegeza masharti ya upataji wa mikopo asilimia nne kwa vijana ili wapate kujiunga kwenye vikundi na kupata mitaji ya kujiajiri wenyewe.
Alisema wakati wanaanza kusoma mafunzo walikuwa 142 lakini wamehitimu wanafunzi 118 huku wanafunzi 24 wakishindwa kumaliza masomo yao kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo utoro sugu pamoja na wengine kuambulia ujauzito na kuacha masomo sababu ya kuishi kwenye magheto.
Aidha Mratibu wa mafunzo chuoni hapo Rashid Ntahigiye alisema wanafunzi hao 118 wamehitimu fani mbalimbali ikiwemo umeme, uselemala, uchomeleaji, ubunifu na ushonaji nguo, ufundi bomba, ujenzi pamoja na mafundi wa mitambo.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Chuo cha Ufundi Stadi Veta mkoani Shinyanga, Magu Mabelele alisema chuo hicho kina jumla ya wanafunzi 400, wasichana wakiwa ni 133 na wavulana 267 huku akitoa wito kwa wazazi wa Shinyanga kupeleka watoto wao chuoni hapo ili kupata ujuzi ambao utatimiza ndoto zao.
Ubunifu katika mitindo.
Imeandaliwa na Marco Maduhu- Malunde 1 Blog
SOMA>>> Habari mbalimbali za Mahafali
No comments: