LIVE STREAM ADS

Header Ads

Shirika la Under The Same Sun latambulisha mradi Kanda ya Ziwa

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Mratibu wa Mradi wa Mfuko wa Canada kwa ajili ya mipango ya kijamii (Canadian Fund For Local Initiative- CFLI) kutoka Shirika la Under The Same Sun, Grace Wabanhu akitambulisha mradi huo kwa wanawake wenye ualbino pamoja na wanawake wenye watoto walio na ualbino katika Mkoa wa Shinyanga.

Na Kadama Malunde, Malunde 1 Blog
Shirika la Under The Same Sun limetambulisha rasmi mradi wa Mfuko wa Canada kwa ajili ya mipango ya kijamii (Canadian Fund For Local Initiative- CFLI) wenye lengo la kuwajengea uwezo wanawake wenye ualbino na wanawake wenye watoto wenye ualbino katika mkoa wa Shinyanga ili wawe na uelewa wa kutosha na kupata ujasiri wa kuielimisha jamii juu ya hali ya ualbino.

Mradi huo umetambulishwa Novemba 18,2019 katika ukumbi wa Shinyanga Fairies Hotel Mjini Shinyanga wakati wa ufunguzi wa warsha ya siku tatu kuhusu elimu ya ualbino kwa na wanawake wenye ualbino na wanawake wenye watoto wenye ualbino 30 kutoka wilaya za mkoa wa Shinyanga.

Mratibu wa mradi huo kutoka Shirika la Under The Same Sun, Grace Wabanhu alisema utadumu katika kipindi cha miezi minne ukitekelezwa katika mikoa ya Shinyanga na Mwanza ukitarajiwa kufikia tamati mwezi Januari 2020.

"Lengo la mradi unaofadhiliwa na watu wa Canada ni kutoa elimu ya ualbino kwa wanawake hawa, tumechukua wanawake 30 kutoka wilaya zote za mkoa wa Shinyanga,Mwanza hivyo hivyo wanawake 30. Wanawake hawa watapata mafunzo ya uelewa juu ya ualbino na wao ndiyo watakuwa wakufunzi kuielimisha jamii" alisema na kuongeza;

"Tunatarajia kwamba wanawake watakaojengewa uwezo watakuwa na uelewa wa kutosha juu ya hali ya ualbino na watakuwa na ujasiri wa kuielimisha jamii inayowazunguka kwa lengo la kuondoa unyanyapaa na ukatili dhidi yao na watoto wenye ualbino ili kuleta usawa kati ya watu wenye ualbino na wasio na ualbino" aliongeza Wabanhu.

Alisema wameamua kuchagua kundi la wanawake wenye ualbino na wanawake wenye watoto wenye ualbino kutokana na kwamba kundi hilo limesahaulika lakini kwa kuzingatia kuwa akina mama hao ndiyo wanalea watoto na ni waathirika wakubwa wa vitendo vya unyanyapaa na ukatili na wamekuwa wakikimbiwa na waume zao.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Watu wenye ualbino mkoa wa Shinyanga (TAS), Eunice Zabron alisema njia pekee ya kukomesha vitendo vya unyanyapaa na ukatili dhidi ya watu wenye ualbino ni kutoa elimu ya kutosha kwa jamii.

Zabron ambaye pia Mwenyekiti wa Idara na Wanawake na Watoto katika Chama cha Watu wenye ualbino Mkoa wa Shinyanga aliipongeza serikali kwa kuendelea kuwa bega kwa bega na watu wenye ualbino huku akibainisha kuwa vitendo vya unyanyapaa vimeendea kupungua kutokana na elimu inayotolewa na vyombo vya habari na wadau mbalimbali kuhusu ualbino.

Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Lilian Kiyenze kwa niaba ya Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Shinyanga aliwataka wanawake hao kutumia vizuri elimu watakayopatiwa kuhusu ualbino ili wakawe chachu ya mabadiliko katika jamii. 
Afisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Lilian Kiyenze akizungumza kwa niaba ya Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Shinyanga.
Wadau wakimsikiliza Afisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Lilian Kiyenze.
Mratibu wa mradi wa Mfuko wa Canada kwa ajili ya mipango ya kijamii, Grace Wabanhu akitoa ufafanuzi kuhusiana na mradi huo.
Mwenyekiti wa Chama cha Watu wenye ualbino Mkoa wa Shinyanga (TAS), Eunice Zabron akizungumza kwenye utambulisho wa mradi huo.
Wanawake wenye ualbino wakifuatilia utambulisho wa mradi huo.
Wadau wakiwa ukumbini wakati wa utambulisho wa mradi huo.

No comments:

Powered by Blogger.