LIVE STREAM ADS

Header Ads

Serikali ya Zanzibar yaridhishwa na mchango wa TASAF

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Na Ahmad Michuzi
fuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) awamu ya tatu kipindi cha pili umejikita zaidi kufanya kazi na walengwa katika masuala ya uimarishaji wa Elimu, Afya pamoja na mafao kwa walemavu waliomo ndani ya Kaya maskini kupitia Shehia mbalimbali Unguja na Pemba. 

Mkurugenzi Mtendaji wa mfuko huo, Ladislaus Mwamanga alisema hayo wakati akitoa taarifa ya matayarisho ya kuanza kwa awamu hiyo katika kikao cha Wakurugenzi na Maafisa wa Taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kilichofanyika Vuga Mjini Zanzibar.

Ladislaus Mwamanga alisema awamu ya tatu kipindi cha pili ambayo Fedha za mfuko huo jumla ya shilingi Trilioni 2.1 sawa na dola za kimarekani Milioni 883 zimeshatiwa saini inategemewa kuwafikia wananchi wote katika Vijiji mbalimbali hadi vile visivyopata huduma ya TASAF na awamu zilizopita. 

Alisema uongozi wa TASAF utasimamia vyema miradi yote iliyopendekezwa na wananchi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa mabwawa ya kufugia samaki pamoja na miundombinu ya umwagiliaji maji kwenye mashamba ya wana TASAF kwa lengo la kuongeza uzalishaji. 

Aidha aliwahakikishia Wakurugenzi na Waratibu hao wa TASAF wa Zanzibar kwamba mafao yote yanayolalamikiwa katika kipindi cha nyuma yatalipwa mapema kabla ya muendelezo wa kipindi cha pili kuanza rasmi.

Mwamanga alifahamisha kwamba yapo mabadiliko ya muundo mzima wa TASAF kipindi cha pili yatakayozingatia zaidi maboresho ya shughuli za mfuko huo ili miradi yake iweze kufanya kazi kwa ufanisi kupitia mfumo wa kisasa wa Mtandao wa mawasiliano katika kutanua wigo wa maendeleo ya kiuchumi. 

Alielezea faraja yake kutokana na mafanikio makubwa ya awamu zilizopita za mfuko huo zilizowezesha wanafunzi 277 wa Kaya maskini Tanzania walipata mikopo ya elimu ya juu kutoka taasisi ya HELB ili waweze kuendelea na masomo yao ya Vyuo Vikuu mwaka 2019. 

Wakitoa michango yao katika kikao hicho walisema TASAF awamu ya yatu kipindi cha pili inapaswa kutoa upendeleo zaidi kwa wananchi wenye mahitaji maalum ili kuwapunguzia utegemezi. 

Wajumbe hao pia wakaelezea changamoto zinazowakumba Watendaji wa mfuko huo ambazo zinapaswa kutafutiwa ufumbuzi wakizitaja kuwa ni pamoja na ucheleweshaji wa taarifa, udanganyifu kwa baadhi ya Watendaji pamoja na ufinyu wa elimu kwa walengwa. 

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mohamed Aboud Mohamed aliushukuru uongozi mzima wa mfuko huo kwa jitihada zake za kuunga mkono miradi ya wananchi katika maeneo mbali mbali Nchini. 

Waziri Aboud aliwakumbusha Viongozi na Watendaji wanaosimamia mfuko huo kuangalia zaidi uimarishaji wa miradi ya maendeleo hasa katika sekta ya elimu na kilimo ambayo inasaidia kukwamua Kaya maskini katika kujiletea maendeleo yao. 

Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Ayoub Mohamed Mahmoud alimkabidhi rasmi Uenyekiti wa Kamati ya Mfuko wa TASAF Unguja Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi, Hassan Khatib Hassan ambapo awali Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Ladislaus Mwamanga alikutana kwa mazungumzo ya kubadilishana mawazo na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Vuga Mjini Zanzibar. 

Katika mazungumzo yao Balozi Seif aliwapongeza Viongozi wa Mfuko wa TASAF kutokana na kazi nzuri wanayoifanya hususan kwa upande wa Visiwa vya Unguja na Pemba kwa kuendeleza kuwatumikia wananchi ili waweze kujikomboa kiuchumi. 

Alitoa rai kwa watumishi hao wa TASAF kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kutokana na faida zinazopatikana kupitia miradi na mafao ya TASAF katika kusukuma gurudumu la maendeleo. Aidha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisisitiza ufuatiliaji wa taarifa sahihi za wananchi ili kuhakikisha kila mstahiki anapatiwa fursa hiyo na kuitumia ipasavyo. 

"Wananchi nao wanapaswa kutoa taarifa sahihi kupitia Sheha wa Shehia zao ili ziweze kusaidia katika ugawaji wa mafao ndani ya Kaya zao" alisisitiza.
Makamu wa pili wa SMZ Balozi Seif Ali Idd akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Ladislaus Mwamanga (wa pili kushoto) juu ya utekelezaji wa shughuli za Mfuko huo.
Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Ladislaus Mwamanga (aliyevaa miwani) akisisitiza jambo kwenye mkutano wa viongozi wa SMZ juu ya utekelezaji wa shughuli za TASAF.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa SMZ, Mohamed Abood akizungumza kwenye kikao cha kuwajengea uelewa viongozi wa SMZ juu ya utekelezaji wa shughuli za TASAF.
Baadhi ya maafisa wa SMZ wakiwa katika kikao cha kuwajemgea uelewa juu ya masuala mbalimbali ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).

No comments:

Powered by Blogger.