LIVE STREAM ADS

Header Ads

Migodi nchini yatakiwa kuwasilisha mipango ya ufungaji

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Waziri wa Madini, Doto Biteko akizungumza kwenye kongamano la kwanza la usimamizi na utunzaji endelevu wa mazingira katika Sekta ya Madini jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila akitoa salamu zake kwenye kongamano hilo.
Washiriki wakifuatilia kongamano hilo.
Washiriki wa kongamano hilo na viongozi mbalimbali wakiwa kwenye picha ya pamoja na Waziri wa Madini, Doto Biteko (wa tatu).

Na Greyson Mwase, Dodoma
Waziri wa Madini, Doto Biteko amezitaka kampuni za madini zinazojihusisha na uchimbaji wa kati na mkubwa kuwasilisha mipango ya ufungaji wa migodi kama Sheria ya Madini na Kanuni zake inavyoelekeza.

Waziri Biteko aliyasema hayo Disemba 16, 2019 jijini Dodoma kwenye kongamano la kwanza la usimamizi na utunzaji endelevu wa mazingira katika Sekta ya Madini linalokutanisha kampuni za madini, taasisi za Serikali na wataalam wa mazingira kutoka taasisi mbalimbali kwa lengo la kubadilishana uzoefu katika usimamizi wa mazingira.

Alisema kwa hapa nchini kuna wamiliki wa migodi mikubwa na ya kati takribani 200 ambao wanastahili kuwa na mipango ya ufungaji migodi (yaani Mine Closure Plans) lakini mpaka sasa ni wamiliki wa migodi kumi sawa na asilimia tano pekee ndiyo wamewasilisha mipango ya ufungaji wa migodi yao.

Aliongeza kuwa kati ya mipango yote 10 iliyowasilishwa, mipango minne tu sawa na asilimia 40 ndiyo ilikidhi vigezo na kuidhinishwa na Serikali na kuendelea kufafanua kuwa mpaka sasa ni migodi mitatu tu sawa na asilimia 1.5 ndio imekwishaweka hati fungani zenye thamani ya dola za kimerekani milioni 41.

Aliongeza kuwa, sambamba na kutakiwa kuwa na mipango ya ufungaji wa migodi, kwa mujibu wa Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 ikisomwa na marekebisho yake ya mwaka 2017 na 2018 mbali na kutakiwa kuwasilisha mipango ya ufungaji migodi, ni wajibu wa kila mmiliki wa leseni kubwa za uchimbaji (Mining License na Special Mining Licence) kuweka dhamana ya ukarabati mazingira ili iweze kutumika kurudishia mazingira yaliyoharibika ikitokea mgodi huo umefungwa ghafla au kutelekezwa bila kufanya ukarabati wa mazingira inavyotakiwa.

Katika hatua nyingine Waziri Biteko alitoa rai kwa wamiliki wa migodi kusimamia vyema mabwawa ya kuhifadhi takasumu na kuongeza kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua kali dhidi ya wamiliki migodi ambao hawasimamii vema mabwawa haya. 

No comments:

Powered by Blogger.