LIVE STREAM ADS

Header Ads

RC Mtaka atoa kongole kwa Shirika la AGPAHI

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Mkuu wa mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka ameipongeza Asasi ya kitaifa isiyo ya kiserikali ya Ariel Glaser Pediatric AIDS Healthcare Initiative (AGPAHI) kwa kutekeleza kikamilifu miradi ya UKIMWI na kuwagusa wananchi moja kwa moja.

Mhe. Mtaka ametoa pongezi hizo Desemba 6,2019 kwenye kikao cha Bodi ya Wakurugenzi wa AGPAHI na wadau wa UKIMWI mkoani Simiyu kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Simiyu. 

Mtaka alisema AGPAHI ni taasisi maarufu mkoani Simiyu kutokana na kwamba imekuwa ikifanya vitu vinavyoonekana katik sekta ya afya mkoani humo kwa kusaidia wananchi. 

“Nawapongeza sana AGPAHI kazi yenu inaonekana,kazi yenu haihitaji tochi ili kuona mnachofanya. Huwezi kuzungumzia mafanikio ya mkoa wa Simiyu kwenye sekta ya afya bila kuwataja AGPAHI”,alisema Mhe. Mtaka. 
“Tunazo taasisi 14 zinazojishughulisha na masuala ya afya mkoani Simiyu. Hawa wadau 13 wangefanya walau robo tu ya kilichofanywa na AGPAHI,tungekuwa na maendeleo makubwa sana katika mkoa wetu na nchi kwa ujumla”,aliongeza Mtaka. 

Mkuu huyo wa mkoa aliipongeza Bodi ya Wakurugenzi wa AGPAHI inayoongozwa na Watanzania kwa kutekeleza miradi inayogusa maisha ya wananchi huku akizitaka taasisi zingine kuiga mfano wa AGPAHI. 

“Wajumbe wa bodi ya AGPAHI mna ujasiri wa kutembelea miradi yenu kwenye mikoa kwa sababu miradi ipo.Nyinyi mna vitu,magari yenu pia yamekuwa yakitusaidia sana.Kuna baadhi ya taasisi hazina ujasiri wa kutembelea miradi kwa sababu hawana miradi,wengine kazi yao ni kugonga semina tu mwaka mzima.Hebu tufanye kazi zinazogusa wananchi tubadilishe mkoa huu”,alieleza Mtaka. 

Katika hatua nyingine Mtaka alisema serikali itaendelea kushirikiana na wadau wote wa maendeleo mkoani humo ili katika kuwaletea maendeleo wananchi. 

Mtaka alitumia fursa hiyo kuwakumbusha wananchi kutumia kondomu ili kupunguza maambukizi ya VVU huku akibainisha kuwa kuwa upo umuhimu wa kuvunja ukimya,vijana waelezwe ukweli kuhusu UKIMWI kwamba upo na unaua hivyo wachukue tahadhari. 

Kwa upande wake,Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya AGPAHI, Dkt. Edith Ngirwamungu alisema AGPAHI inatekeleza miradi yake ya UKIMWI kwa kushirikiana na serikali lengo likiwa ni kuhakikisha fedha zinazotolewa na wafadhili zinawanufaisha watanzania. 

“Tunaushukuru mkoa wa Simiyu kwa ushirikiano mnaotupatia,tunajitahidi kufanya kazi kuwafikia wananchi,AGPAHI tunataka mtoto asizaliwe na maambukizi ya VVU,hivyo tutaendelea kushirikiana na serikali katika kutoa huduma za VVU na UKIMWI kwa wananchi”,alisema Dkt. Ngirwamungu. 

Alisema AGPAHI inaendelea kuongeza ubora na upatikanaji wa huduma za matunzo na tiba za VVU kwa watoto wachanga,vijana na watu wazima katika mikoa ya Simiyu,Mwanza,Mara na Shinyanga. 

Meneja Miradi AGPAHI mkoa wa Simiyu Dkt. Julius Sipemba alisema AGPAHI inatoa huduma za VVU na UKIMWI kwa mkoa mzima wa Simiyu ambapo Mkoa wa simiyu una vituo 233 vya kutolea huduma za afya na 73 kati ya hivyo hupata usimamizi wa moja kwa moja kutoka AGPAHI. 

Alisema wagonjwa wanaopata huduma kwenye vituo 73 ni sawa na 95% ya wagonjwa wote walioko kwenye vituo 233. "AGPAHI inaboresha miundombinu kwa kujenga na kukarabati majengo, huduma za maabara kwa kununua madawa na vifaa 'iliwezesha maabara za wilaya kutoka nyota moja mpaka tatu', imetoa magari mapya kwa halmashauri 4 kati ya 6, imetoa pikipiki, msaada wa kuchunguza kifua kikuu, Saratani ya mlango wa kizazi",alieleza Dkt. Sipemba. 

Aliongeza kuwa AGPAHI pia inaajiri watoa huduma wa afya kwenye maeneo yenye uhitaji na inatoa mafunzo kwa watoa huduma kulingana na miongozo ya wizara ya afya. 

Wakiwa mkoani Simiyu,Wajumbe wa bodi ya Wakurugenzi ya AGPAHI wametembelea Kituo cha Tiba na Matunzo cha Hospitali ya wilaya ya Bariadi,kukutana na Mganga Mkuu wa mkoa wa Simiyu na Mkuu wa mkoa wa Simiyu pamoja na wadau wa VVU na UKIMWI mkoani Simiyu. 
Mkuu wa mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka akizungumza katika kikao cha Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa AGPAHI na wadau wa afya mkoani Simiyu Desemba 6,2019. Kushoto ni Mkurugenzi wa AGPAHI, Dkt. Sekela Mwakyusa,kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya AGPAHI, Dkt. Edith Ngirwamungu.
Mkuu wa mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka akiipongeza AGPAHI kwa huduma za VVU na UKIMWI inazotoa mkoani Simiyu.
Katibu Tawala mkoa wa Simiyu mhe. Jumanne Sagini akiipongeza AGPAHI kwa kutekeleza miradi inayogusa wananchi mkoani Simiyu.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya AGPAHI, Dkt. Edith Ngirwamungu akizungumza katika kikao cha wadau wa afya na kueleza kuwa AGPAHI itaendelea kushirikiana na serikali katika kutoa huduma za VVU na UKIMWI.
Mkurugenzi wa AGPAHI, Dkt. Sekela Mwakyusa akielezea shughuli zinazofanywa na AGPAHI mkoani Simiyu.
Awali Mkurugenzi wa AGPAHI, Dkt. Sekela Mwakyusa akiwashukuru viongozi wa mkoa wa Simiyu kwa kuendelea kushirikiana na AGPAHI katika kutekeleza miradi ya VVU na UKIMWI.
Meneja Miradi AGPAHI mkoa wa Simiyu Dkt. Julius Sipemba akiwasilisha mada kuhusu shughuli zinazofanywa na asasi ya AGPAHI mkoani Simiyu.
Mkuu wa wilaya ya Bariadi Mhe. Festo Kiswaga akichangia hoja wakati wa kikao cha wadau wa afya mkoani Simiyu.
Mganga Mkuu wa mkoa wa Simiyu Dkt. Festo Dugange akichangia hoja wakati wa kikao cha wadau wa afya mkoani Simiyu.
Kikao kinaendelea.
Kijana James Leonard akielezea jinsi alivyonufaika na Klabu za watoto na vijana zinazohudumiwa na AGPAHI. Aliwataka vijana wajitokeze kupima afya zao na pale wanapobainika kuwa na maambukizi ya VVU basi watumie dawa za kufubaza makali ya VVU kwani kuwa na maambukizi ya VVU siyo mwisho wa maisha.
Minza Manyama akiwahamasisha wazazi na walezi kuwa wawazi kwa watoto waliozaliwa na maambukizi ya VVU. Alitumia fursa hiyo kuipongeza AGPAHI kwa huduma za VVU na UKIMWI inazoendelea kutoa kwa wananchi.
Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya AGPAHI wakiwa kwenye kikao cha wadau wa afya mkoani Simiyu.
Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya AGPAHI wakiwa kwenye kikao cha wadau wa afya mkoani Simiyu.
Wajumbe wa bodi ya wakurugenzi ya AGPAHI wakiwa nje ya kituo cha Tiba na Matunzo cha Hospitali ya wilaya ya Bariadi. 
Picha ya pamoja uongozi wa mkoa wa Simiyu,AGPAHI na wadau wa afya mkoani Simiyu.
Picha ya pamoja uongozi wa mkoa wa Simiyu,AGPAHI na wanufaika wa miradi inayotekelezwa na AGPAHI mkoani Simiyu.
Picha ya pamoja uongozi wa mkoa wa Simiyu na AGPAHI.
Na Kadama Malunde - Malunde 1 Blog

No comments:

Powered by Blogger.