LIVE STREAM ADS

Header Ads

Matapeli 'wavamia' zoezi la usajili laini za simu

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Judith Ferdinand, BMG
Wananchi wametakiwa kutokutoa namba za siri za huduma za kifedha ikiwemo mitandao ya simu na akaunti za benki kwa watu wanaohusika na usajili wa laini za simu kwa njia ya alama za vidole.

Hii ni baada ya kuibuka kundi la watu waliobuni mbinu mpya ya kutumia fursa hiyo kufanya utapeli jijini Mwanza kwa kuwashawishi kuwa usajili wa laini za simu kwa alama za vidole na kitambulisho cha Taifa unaendana na uhakiki wa akaunti ya benki.

Mkuu wa Mamalaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Kanda ya Ziwa, Francis Mihayo alisema baada ya zoezi la usajili kuongezewa muda hadi Januari 20, 2020 kumeibuka kundi la vijana linaloingia mtaani kuwatapeli wananchi.

Mihayo aliyasema hayo Januari 03, 2020 kwenye kikao kazi cha kutoa taarifa ya hali ya mawasiliano Kanda ya Ziwa kilichowajumuisha viongozi wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Ilemela na Nyamagana, Afisa Usajili kutoka Mamlaka ya Taifa ya Vitambulisho NIDA, watoa huduma wa makampuni ya simu pamoja na waandishi wa habari.

Aliongeza kuwa vijana hao wanakuwa wamevalia sare za watoa huduma kutoka makampuni ya mitandao ya simu hupita majumbani, mitaani na sehemu za biashara na kuwalaghai baadhi ya wananchi kuwa usajili wa namba za simu kutumia alama za vidole unafanyika sambamba na uhakiki wa akaunti za Benki kitendo hicho usababisha watu wengi kuibiwa fedha zao kwa kutumia mitandao.

"Baada ya Mhe. Rais kuongeza muda wa usajili tumebaini kuongezeka wimbi la utapeli unaofanywa na wakala wao wasio waamininifu hivyo waananchi watambue zoezi linaloendelea ni la usajili wa laini za simu kwa njia ya kibiometria kwa kutumia kitambulisho cha Taifa au namba ya kitambulisho cha Taifa na siyo uhakiki wa akaunti za benki hivyo akitokea mtu anayemtaka kufanya hivyo atoe taarifa mapema" alisema Mihayo.

Aidha alisema takwimu zinaonyesha hadi Desemba 31, 2019 idadi ya laini zilizosajiliwa ni 48,321,949 ambapo laini zilizosajiliwa kwa alama za vidole ni 24,021,757 sawa na asilimia 49.7 ya laini zote huku laini ambazo hazijasajiliwa kwa alama za vidole zikiwa ni 24,300,192 hivyo wananchi waendelee kujitokeza kwa wingi ili kujisajili kabla ya muda wa mwisho ulioongezwa na Rais Dkt. John  Magufuli.

Naye Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Nyamagana, Mrakibu wa Polisi Juma Jumanne alisema utapeli wa mitandao ya simu umeanza muda mrefu na unabadilika kutokana na wakati lakini usajili wa alama za vidole ulisaidia kupunguza matukio hayo lakini baada ya siku za usajili kuongezwa makosa ya vitendo vya utapeli vimeongezeka hivyo wananchi wachukue tahadhari na wawe makini na vijana hasa wale wanaokuwa karibu nao kila wakati pia wasipende urahisi wa maisha ama biashara.

Kwa upande wake Raphael Manase ambaye ni Afisa Msajili wa NIDA Mkoa wa Mwanza aliwataka wananchi kuzingatia maelekezo wanayopewa na kufuata utaratibu uliopo pamoja na kutokukubali kupewa maelekezo mengine ya upotoswaji kitu ambacho kitasababisha kutapeliwa.

No comments:

Powered by Blogger.