LIVE STREAM ADS

Header Ads

Waziri Biteko amaliza mgogoro Kahama

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Waziri wa Madini, Doto Boiteko akizungumza na wachimbaji wadogo wa madini katika Kijiji cha Mwabomba, Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga.
Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Mwabomba wilayani Kahama wakimsikiliza Waziri Biteko (hayuko pichani).
Na Asteria Muhozya, Kahama
Tume ya Madini imeagizwa kuitisha kikao cha Kamati ya Ufundi ili kupitia upya mchakato wa leseni nne za uchimbaji madini za Balafuma, namba 1, namba 2, na namba 6 katika Kijiji cha Mwabomba Kata ya Idahina Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga ili kupatiwa wachimbaji wadogo badala ya kampuni ya Calton Miyabi (T) Ltd. 

Uamuzi huo umefikiwa baada ya kuwepo kwa mgogoro wa leseni ya uchimbaji katika maeneo hayo kati ya wachimbaji wadogo wa madini na kampuni za uchimbaji uliodumu kwa miaka 20. 

Waziri wa Madini, Doto Biteko alitoa agizo hilo Mei 23, 2020 wakati wa ziara yake kijijini hapo ya kukagua shughuli za uchimbaji madini, kuzungumza na wananchi na kampuni hiyo na kueleza kwamba, wachimbaji hao wanayo haki ya kumiliki eneo husika kutokana na aina ya makubaliano yaliyofanyika awali kati ya Wachimbaji na Kampuni ya Tanzania Minerals Liquefied Gas and Petroleum Limited . 

Biteko aliongeza kuwa, anafahamu mchakato wa leseni hizo kupatiwa kampuni ya Calton Miyabi (T) Ltd ulifika mbali lakini hauna budi kupitiwa upya na kamati husika na maombi ya leseni hizo asipewe mtu mwingine isipokuwa wachimbaji wadogo wa eneo hilo. 

Hata hivyo aliishauri kampuni husika kufanya mazungumzo na wachimbaji hao endapo kuna shughuli za uchimbaji mkubwa uliopangwa kufanyika, huku ikitakiwa kukumbuka kuwa wachimbaji hao ndiyo wamiliki halali wa maeneo husika. 

Waziri Biteko aliwapongeza wachimbaji wa Mwabomba na kusema kuwa, kwa kipindi kifupi wameweza kulipa kodi za Serikali zaidi ya Shilingi Milioni 500 huku wakichangia huduma za kijamii zenye thamani ya shilingi milioni 500. 

Aidha alitumia fursa hiyo kuwaasa wachimbaji kuhakikisha wanaanzisha vitega uchumi vingine kutokana na faida wanazopata kufuatia shughuli za uchimbaji madini wanazozifanya na kueleza kuwa, kuna wakati madini yanakwisha. 

"Lakini pia wale wachimbaji wanaochimba kwa midomo waache kuwachanganya wachimbaji na kutafuta migogoro. Heshima ya Sekta hii ni kutokuwepo migogoro, lakini pia Mhe. Rais anataka kutengeneza mamilionea siyo migogoro" alisema Waziri Biteko 

Vilevile Waziri Biteko aliwakumbusha wachimbaji nchini hususan katika kipindi hiki cha Ugonjwa wa Covid-19, kuhakikisha wanafanya shughuli zao kwa kuendelea kuchukua tahadhari juu ya ugonjwa huo huku wakiwalinda wengine. 

"Jitahidini kuishi salama, jilinde wewe na uwalinde na wengine na hakikisha muda wote upo salama. Usipokuwa salama hata madini hayo hutochimba na waziri hawezi kuja" alisisitiza Waziri Biteko. 

Waziri Biteko alielezea kwa kifupi mazingira yaliyosababisha kuwepo kwa mgogoro huo ambapo ameeleza kuwa, awali, kabla ya kampuni ya Calton Miyabi (T) Limited, kampuni ya Tanzania Minerals Liquidfied Gas and petroleum Limited iliingia makubaliano na wachimbaji na kutoa maeneo Manne baadaye ikachukua leseni kwa jina la Tanzania Minerals bila kujumuishwa wachimbaji hao na baada ya mwaka mmoja leseni ikafutwa na kupewa kampuni ya kigeni na hatimaye kampuni ya Australia iliyoomba leseni ya utafiti. 

Awali Waziri Biteko alizitaja juhudi za Serikali zilizofanywa katika Awamu ya Tano za kuhakikisha inawafanya watanzania kuwa sehemu ya wamiliki wa uchumi wa madini, wachimbaji nchini kufanya shughuli zao vizuri ikiwemo biashara ya madini kwa kuanzisha Masoko ya Madini mikoa mbalimbali nchini suala ambalo limewezesha wachimbaji kupata maeneo maalum ya kuuza madini yao.

Kwa upande wake Katibu Tawala Wilaya ya Kahama Timoth Ndanya alimshukuru Waziri Biteko kwa kumaliza mgogoro huo na kuchukua nafasi hiyo kuendelea kuwasisitiza wachimbaji hao kuzingatia maelekezo ya Wizara ya Afya kuhusu ugonjwa wa Covid -19. 

Naye Diwani wa Kata ya Idaiya, Yuda Majonjozi amesema alimpongeza Waziri Biteo kwa kutambua uwepo wa wachimbaji wadogo katika eneo lake na kueleza kuwa, wachimbaji wamekuwa wakichangia katika maendeleo ya kijiji kwa kuchangia huduma za kijamii. 

"Mhe. Waziri, Mhe, Rais alitwambia katika eneo hili hatutafukuzwa tena, tunashukuru sana leo tumefikia suluhisho ya mgogoro huu" alisema Majonjozi.

No comments:

Powered by Blogger.