LIVE STREAM ADS

Header Ads

Biteko ataka mradi wa dhahabu Singida kuanza mara moja

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Waziri wa Madini Doto Biteko ameieleza Kampuni ya Shanta Mining Company Limited kuwa inao wajibu wa kuhakikisha Mradi wa Uchimbaji Dhahabu wa Singida Resources PLC unaanzishwa kutokana na manufaa yake kiuchumi ikiwemo kuifungamanisha Sekta ya Madini na sekta nyingine na kiu ya wananchi kuona mradi huo ukitekelezwa.

Waziri Biteko ameyasema hayo Mei 13, 2020 jijini Dodoma wakati wa kikao kilichofanyika kwa njia ya Video Conference baina yake na Watendaji wa Wizara na Tume ya Madini, Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Edward Mpogolo, Kampuni ya Shanta Mining na Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE). 

Kikao hicho kimefanyika ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa ambapo kampuni hiyo iliwasilisha kwake masuala kadhaa yaliyolenga kuendeleza mradi huo.

Kikao hicho kimeyataja masuala hayo kuwa ni pamoja na mpango wa Shanta Mining kujiorodhesha kwenye soko la Hisa la Dar es Salaam, Mpango wa Shanta Mining kuuza sehemu ya Hisa zake zilizopo kwenye mradi wa Singida Resources PLC kupitia DSE pamoja na hatua zilizofikiwa katika ulipaji wa fidia kwa wananchi wenye umiliki wa ardhi ili kupisha mradi huo.

Aidha, Waziri Biteko ametumia kikao hicho kuipongeza kampuni husika na kueleza kuwa imekuwa ikifuata vizuri utekelezaji wa maagizo ya Serikali na hivyo kutumia fursa hiyo kuitaka kupokea ushauri ulitolewa katika kikao hicho na kuufanyia kazi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Edward Mpogolo, ameisisitiza kampuni hiyo kuhakikisha inatekeleza mradi huo ikiwemo kuzingatia matakwa ya kisheria wakati wa utekelezaji wake.

Naye, Meneja Mkuu wa Kampuni ya Shanta Mining Philbert Rweymamu, amemwakikishia Waziri Biteko kuwa kampuni hiyo itahakikisha mradi huo unatekelezwa katika muda uliopangwa na kuiomba wizara kuisaidia kampuni hiyo kufikia malengo yake.

“Mhe. Waziri nia na madhumuni yetu ni kuhakikisha mradi unaanza mwaka huu,” amesisitiza Rweymamu.

No comments:

Powered by Blogger.