MWANZA “Kalemani aagiza wananchi kuunganishiwa umeme”
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Waziri wa
Nishati, Dkt. Medard Kalemani amegoma kuwasha umeme katika Kijiji cha Isamilo
kilichopo Wilaya Misungwi mkoani Mwanza baada ya kukuta nyumba tatu kati ya 121
katika Kijiji hicho ndizo zimeunganishiwa na nishati hiyo.
Dkt.
Kalemani amefikia maamuzi hayo Juni 26, 2020 alipofanya ziara ya kikazi
wilayani Misungwi kufuatilia na kukagua utekelezaji wa mradi ya usambazaji
umeme vijijini (REA) na kueleza kutoridhishwa na kasi ya mkandarasi aliyepewa
kazi hiyo.
Kutokana na
hatua hiyo, Dkt. Kalemani aliwaagiza viongozi wa TANESCO Wilaya Misungwi na
Mkoa Mwanza kuhakikisha kazi ya kuunganisha nishati ya umeme katika nyumba
zilizosalia inaanza kesho Juni 27, 2020 ili baada ya wiki moja arudi kijijini
hapo kuwasha rasmi nishati hiyo.
“Mkandarasi (NIPO GROUP) aliyekuwa anasambaza
umeme katika Mkoa Mwanza ameshindwa kazi ambapo wiki iliyopita tumemfuta na kuikabidhi
kwa shirika la umeme ETOCO. Tulimpa vijiji 127 lakini ameshindwa kusambaza
umeme katika vijiji 70 kwani mkataba wake ulikuwa unaisha Juni 30, 2020”
alisema Dkt. Kalemani.
Aidha Dkt.
Kalemani alieleza kusikitishwa na hatua ya vijiji 41 kati ya 114 wilayani
Misungwi kutojumuishwa kwenye mpango wa kuunganishiwa umeme na kuwatoa hofu
wakazi wa vijiji hivyo kwamba watafikishiwa nishati hiyo haraka iwezekanavyo.
Hata hivyo
baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Isamilo wilayani Misungwi akiwemo Bi. Restuta
Wilbert wameeleza kuwa na matumaini makubwa ya nyumba zao kuunganishiwa umeme
baada ya nishati hiyo kufikishwa kijijini hapo.
“Mimi tangu
kuzaliwa umeme nilikuwa nauona tu mbali hivyo nashukuru sana kuuona kwenye
maeneo yetu na naomba kazi aliyoisema (Dkt. Kalemani) waitekeleze ili tupate
umeme” alisisitiza Bi. Restuta.
Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (kulia) akizungumza na wakazi wa Kijiji cha Isamilo wilayani Misungwi (hawako pichani). Kushoto ni Katibu Tawala Wilaya Misungwi, Petro Sabatto aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya, Juma Sweda.
Tazama BMG ONLINE TV hapa chini
SOMA>>> Habari kuhusiana na TANESCO
No comments: