LIVE STREAM ADS

Header Ads

Ufahamu wa Fomu Namba Tatu (PF3) bado ni changamoto kwa wananchi

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Na Edwin Soko, Buchosa
Baadhi ya wakazi wa Halmashauri ya Buchosa wilayani Sengerema wamekiri kutoielewa vyema Fomu Namba Tatu (PF3) inayotolewa polisi kutokana na uelewa mdogo uliopo katika jamii.

Waliyasema hayo hivi karibuni waliotembelea na waandishi wa habari waliokuwa wanafuatilia utekelezaji wa mradi wa BORESHA unaotekelezwa kwenye Halmashauri hiyo kupitia umoja wa taasisi za kidini nchini (TIP).

Mmoja wa wakazi hao, Geofrey Zakaria alisema haifahamu fomu hiyo kwani hajawai kuiona ama kutambua muhimu wake ambao ni pamoja na kutumika kama ushahidi kwenye makosa ya kijinai ikiwemo ukatili wa kijinsia.

Naye Doricus Renatus alisema wananchi kukosa uelewa juu ya fomu hiyo kunatokana na kutokuwepo kwa juhudi za kutosha za kuwaelimisha ili kuifahamu na kutambua umuhimu wake huku Kabula Michael ambaye alikiri kuisikia akisema inatumika kwenye matukio ya ukatili/ shambulio lakini bado hafahamu umuhimu wake ambao ni pamoja na kutumika kama ushahidi mahakamani.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa taasisi ya usaidizi wa kisheria Buchosa (Womenkind and Protection Organization- BUWOPA), Faida Kalokozi alibainisha kuwa moja ya changamoto ya "PF3" ni jamii kutokuwa na uelewa wa fomu hiyo na hivyo kusababishwa kesi nyingi za ukatili ikiwemo wa kingono kupoteza ushahidi mahakamani.

Taasisi ya TIP inayoundwa na taasisi nne za kidini ikiwemo BAKWATA, CCT, TEC na MoZ inatekeleza mradi wa kuzuia ukatili wa kingono kwa watoto katika Halmashauri ya Buchosa na moja ya changamoto zilizobainika ni jinsi "PF3" zinavyopoteza ushahidi na kusababisha haki za watoto kupotea mahakamani kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kukosewa kujazwa.

Kupitia mradi wa BORESHA, wananchi na wasaidizi wa kisheria ngazi ya jamii katika Halmashauri ya Buchosa wamejengewa uwezo ili kuitambua fomu hiyo (PF3) na umuhimu wake.

No comments:

Powered by Blogger.