LIVE STREAM ADS

Header Ads

Waandishi wa Habari Kanda ya Ziwa wapewa mafunzo na TASAF

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF) umetoa mafunzo kwa waandishi wa habari Kanda ya Ziwa kwa lengo la kuwajengea uelewa kuhusu utekelezaji wa shughuli za mfuko huo katika kipindi cha pili awamu ya tatu (PSSN III) ili wakawaelimishe wananchi kupitia vyombo vyao vya habari.

Mafunzo hayo ya siku mbili kuanzia Jumatatu Septemba 28, 2020 yanafanyika jijini Mwanza yakijumuisha waandishi wa habari wa magazeti, redio, runinga na mitandao ya kijamii kutoka mikoa ya Mara, Simiyu, Kagera na Mwanza. 

Akizungumza kwenye mafunzo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Ladislau Mwamanga alisema utekelezaji wa shughuli za TAFAS katika kipindi cha pili awamu ya kwanza na ya pili umekuwa na mafanikio makubwa kwa wananchi kwani wengi wao wameweza kujikwamua kiuchumi kupitia ruzuku walizopokea na kuanzisha miradi ya maendeleo. 

Mwamanga alisema fedha za ruzuku zinazotolewa na TASAF kwa kaya maskini nchini zimesaidia wananchi kuanzisha miradi mbalimbali ikiwemo kilimo, ufugaji na biashara ndogo ndogo na hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi. 

“Fedha za ruzuku kutoka TASAF zimesaidia upatikanaji wa chakula kwa kaya maskini ambapo viwango vya lishe pia vimeboreshwa hususani kwa watoto chini ya miaka mitano huku kaya nyingi zikijiunga na mfuko wa bima ya afya ya CHF iliyoboreshwa” aliongeza Mwamanga. 

Naye Mkurugenzi wa Tathmini na Ufuatiliaji wa Miradi ya TASAF, Fariji Mishael alisema bila mpango wa TASAF nchini kungekuwa na ongezeko la umaskini kwa asilimia mbili kutoka asilimia 28 hadi 30 hivyo mikakati zaidi inahitajika ili kuhakikisha wanufaika hawarudi kwenye umaskini kwa kuwaelimisha na kuwajengea uwezo ili miradi waliyoianzisha iwe endelevu. 

Awali Mtaalamu wa Mawasiliano TASAF, Zuhura Mdungi alisema waandishi wa habari ni miongoni mwa wadau muhimu ambao baada ya kujengewa uelewa watasaidia kuelimisha wananchi kuhusu utekelezaji wa kipindi cha pili cha TASAF awamu ya tatu (PSSN III) kilichozinduliwa rasmi mwezi Februari 2020 na Rais Dkt. John Magufuli jijini Dar es salaam. 

“Baada ya kuelezana utekelezaji wa shughuli za TASAF tutakwenda pia kuwaona walengwa ili kujua mafanikio gani yamefikiwa. Tushirikiane vyema kujengeana uelewa na ufanisi kwa pamoja ili tukawaekimishe pia na wengine” alisisitiza Mdungi. 

Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo, Beresi China kutoka ITV mkoani Simiyu pamoja na Clara Matimo kutoka Mtanzania mkoani Mwanza walisema mpango wa TASAF umekuwa na mchango mkubwa katika jamii ikiwemo kusaidia wanafunzi kutoka kaya maskini kupata elimu hivyo jitihada zaidi iendelee kufanyika ili kuhakikisha fedha za ruzuku hazituki vibaya kama ilivyokuwa hapo awali ambapo baadhi walizitumia kunywea pombe huku pia kukiwa na wanufaika hewa.

Kipindi cha Pili cha TASAF awamu ya tatu kilichoanza mwaka 2020 hadi 2023 kinalenga kuimarisha mafanikio yaliyopatikana na kuwafikia wananchi ambao awali hawakufikiwa ambao ni sawa na asilimia 30 katika Mitaa, Vijiji na Shehia nchini Tanzania.
Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Ladislau Mwamanga.
Naye Mkurugenzi wa Tathmini na Ufuatiliaji wa Miradi ya TASAF, Fariji Mishael.
Waandishi wa habari Kanda ya Ziwa wakifuatilia mafunzo hayo.

No comments:

Powered by Blogger.