LIVE STREAM ADS

Header Ads

SHIRIKA LA CAMFED LAWANOA WASICHANA WALIOKATISHA MASOMO

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Shirika la ufadhili wa masomo kwa watoto wa kike wanaoishi katika mazingira magumu (CAMFED) limetoa mafunzo kwa wasichana walio nje ya mfumo wa shule kwa lengo la kuwajengea uwezo ili kutimiza ndoto zao.

Mafunzo hayo ya siku mbili kuanzia Jumatatu Novemba 16, 2020 yanafanyika katika ukumbi wa Gandhi (Gandhi Hall) yakiwajumuisha zaidi ya wasichana 100 kutoka Halmashauri za Jiji la Mwanza, Manispaa ya Ilemela, Manispaa ya Kahama pamoja na Shinyanga Mji ambao walioshindwa kuhitimu elimu ya kidato cha nne kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo ujauzito. 

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mkurugenzi wa shirika la CAMFED, Lydia Wilbard amesema baada ya wasichana hao kutemwa na mfumo rasmi wa elimu nchini ni vyema kukaa nao na kujadili kwa pamoja mbinu za kuwasaidia kusonga mbele ili kutimiza ndoto zao. 

Amesema wasichana hao wanayo nafasi ya pili kupitia mfumo usio rasmi ambapo wanaweza kujiunga na taasisi mbalimbali ikiwemo VETA na kupata ujuzi wa kuwawezesha kujikwamua kiuchumi ama hata kurejea kwenye mfumo rasmi wa elimu na kuendelea na masomo zaidi. 

Aidha Wilbard ameongeza kuwa wasichana hao pia wanapewa elimu ya afya ya uzazi na HIV/ UKIMWI ili kuwasaidia kujilinda na vishawishi mbalimbali wanavyoweza kukumbana navyo mitaani huku wakiwa mabalozi wazuri kwa wasichana wengine. 

Baadhi ya washiriki wameishukuru CAMFED kwa kuwasaidia kupata mafunzo mbalimbali kupitia VETA hatua ambayo imewatoa kwenye hali ya kukata tamaa na kuweka malengo ya kuhakikisha wanatimiza ndoto zao maishani.
Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
Mkurugenzi wa shirika la CAMFED, Lydia Wilbard akizungumza wakati wa mafunzo hayo.
Mwakilishi wa Mganga Mkuu Mkoa Mwanza akitoa salamu zake kwenye mafunzo hayo.
Mratibu wa CAMFED Mkoa Mwanza, Marry Nziku.
Washiriki wa mafunzo hayo.
Tazama BMG ONLINE TV hapa chini

No comments:

Powered by Blogger.