LIVE STREAM ADS

Header Ads

TAHA yahimiza watanzania kutoogopa soko la Afrika Mashariki

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Taasisi ya kilimo cha bustani TAHA ((Tanzania Horticultural Association) imewahimiza wakulima nchini Tanzania kutoogopa ushindani na badala yake kuchangamkia fursa ya soko la mazao yao katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. 

Rai hiyo ilitolewa na Meneja Miradi wa taasisi hiyo, Eliachea Shang’aa wakati akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya mkulima shambani iliyofanyika Disemba 08, 2020 kwa Mkoa Mwanza katika eneo la Isanzu wilayani Ilemela. 

Shang’aa alisema kuna fursa nyingi katika sekta ya kilimo hivyo ni vyema wakulima wa Tanzania wakathubutu na kutoliogopa soko la shirikisho la Afrika Mashariki wakidhani wenzao wanajua zaidi kuliko wao. 

“Tufumbue macho na tuwe tayari kuthubutu bila kuliogopa shirikisho la Afrika Mashariki kwani tuna raslimali zaidi yao, tuna ardhi ya kutosha pamoja na wataalamu wa kutusaidia” alisisitiza Shang’aa. 

Aidha aliwahimiza wakulima hususani wa mboga, viungo, matunda na maua kutunza kumbukumbu zao za kifedha ili kuondokana na changamoto ya kukosa sifa za kukopesheka kwenye taasisi za kibenki kwani bado kuna changamoto ya mitaji kwa baadhi ya wakulima. 

Naye Afisa Tawala Wilaya Ilemela, Neema Kipeja aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya hiyo, Dkt. Severine Lalika alisema zaidi ya asilimia 80 ya watanzania wanategemea shughuli za kilimo hivyo Serikali imeweka mazingira rafiki kwa wadau ikiwemo TAHA ili kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi ikiwemo kuwajengea uwezo wakulima ili wazalishe kwa tija. 

“Serikali imeondoa tozo mbalimbali kwenye mazao na pembejeo za kilimo ili kuwahamasisha wananchi kujikita kwenye shughuli za kilimo huku ikiwaunganisha pia na taasisi za kifedha ili kupata mikopo yenye riba nafuu na kuondokana na changamoto ya mitaji” alisema Kipeja. 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa kikundi cha wakulima cha Jitegemee Isanzu, Shaban Lukona alisema elimu waliyopewa na TAHA kupitia mradi wa vijana, maisha na kazi unaofadhiliwa na shirika la Plan Intanational imewasaidia kulima kwa tija na kuondokana na changamoto ya ukosefu wa ajira. 

“TAHA wamejitahidi sana kutupatia elimu, ukiwapigia simu wanafika haraka na kutushauri tunapokuwa na changamoto kama mazao kushambuliwa na wadudu ambapo hutushauri aina ya dawa na namna ya kuitumia” alibainisha Lukona akiongeza kuwa TAHA pia imewasaidia kuwaunganishia mfumo wa umwagiliaji kwa njia ya matone, upatikanaji wa masoko pamoja na pembejeo za kilimo. 

Siku ya mkulima shambani huwakutanisha pamoja wakulima ambao ni wanachama wa taasisi ya TAHA ili kujifunza teknolojia na mbinu bora za kilimo kupitia shamba darasa wakulima ambapo kwa Mkoa Mwanza imeshirikisha wakulima kutoka wilaya za Magu, Misungwi, Nyamagana na Ilemela.
Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
Meneja Miradi wa taasisi hiyo, Eliachea Shang’aa akieleza namna taasisi hiyo inavyowasaidia wakulima kushiriki katika kilimo chenye tija ili kunufaika na soko la ndani na nje ya nchi.
Bwana Shamba Kiongozi kutoka taasisi ya TAHA, Giriad Daniel alisema hadi sasa taasisi hiyo inafanya kazi katika mikoa 23 nchini Tanzania ambapo inawajengea uwezo wakulima ili kuingia kwenye sekta ya kilimo pamoja na kuwaunganisha na masoko.
Mwenyekiti wa kikundi cha Jitegemee Isanzu, Shaban Lukona (kushoto) akiongea na wanahabari namna TAHA ilivyowasaidia vijana kujikwamua kiuchumi kupitia kilimo cha tikiti maji.
Mwenyekiti wa kikundi cha Jitegemee Isanzu, Shaban Lukona (kushoto) akiwaeleza wanachama wa TAHA mbinu mbalimbali za kilimo.
Mwenyekiti wa kikundi cha Jitegemee Isanzu wilayani Ilemela, Shaban Lukona akiwa shambani.
Wanachama wa TAHA mkoani Mwanza wakijifunza mbinu mbalimbali za kilimo katika shamba darasa la kikundi cha Jitegemee Isanzu wilayani Ilemela ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya mkulima shambani 2020.
Siku ya mkulima shambani hulenga kutoa elimu na mbinu mbalimbali za kilimo kwa wanachama wa TAHA ili kulima kwa tija.
Shamba darasa la kikundi cha Jitegemee Isanzu wilayani Ilemela.
Bwana Shamba Kiongozi kutoka taasisi ya TAHA, Giriad Daniel (wa tatu kulia) akifafanua jambo kwa Afisa Tawala Wilaya Ilemela, Neema Kipeja (wa pili kushoto) baada ya kutembelea shamba darasa la kikundi cha Jitegemee Isanzu.
Meneja Miradi wa taasisi hiyo, Eliachea Shang’aa (kulia) akifafanua jambo kwa Afisa Tawala Wilaya Ilemela, Neema Kipeja (wa pili kulia) kuhusiana na kilimo cha mboga, matunda, viungo na maua.
Bwana Shamba Kiongozi kutoka taasisi ya TAHA, Giriad Daniel (wa pili kushoto) akifafanua jambo kwa Afisa Tawala Wilaya Ilemela, Neema Kipeja (wa pili kulia)
Mtaalamu kutoka taasisi ya TAHA, Loveness Rugiga (kulia) akitoa elimu kwa wanachama wa taasisi hiyo kwenye maadhimisho ya siku ya mkulima shambani.
Afisa Masoko kutoka TAHA, Reuben Hiza (kulia) akitoa elimu kwa wanachama wa taasisi hiyo kwenye maadhimisho ya siku ya mkulima shambani.
Wanachama wa TAHA mkoani Mwanza wakijifunza mbinu mbalimbali za kilimo chenye tija.
Meneja Miradi wa taasisi hiyo, Eliachea Shang’aa akizungumza kwenye maadhimisho hayo.
Mgeni rasmi, Afisa Tawala Wilaya Ilemela, Neema Kipeja akizungumza kwenye maadhimisho hayo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya Ilemela.
Vijana wa kikundi cha Jitegemee Isanzu wilayani Ilemela.
Mwakilishi kutoka shirika la Plan International linalofadhili mradi wa vijana, maisha na kazi alisema mradi huo unalenga kuwainua vijana ili kujikwamua kiuchumi kupitia shughuli mbalimbali ikiwemo kilimo.
Mtaalamu kutoka TAHA akisisitiza jambo kwenye maadhimisho hayo.
Wanachama wa TAHA wakisoma majarida mbalimbali yanayotoa elimu kuhusiana na kilimo.
Wanachama wa TAHA wakiwa kwenye maadhimisho hayo.
Taswira ya maadhimisho hayo.
Picha ya pamoja.
Tazama BMG TV hapa chini

No comments:

Powered by Blogger.