LIVE STREAM ADS

Header Ads

Mbunge wa Butiama asaidia ukarabati miundombinu ya Shule ya Chief Ihunyo

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Jumla ya kiasi cha shilingi 5,180,000/= ambacho kimetolewa na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Butiama Jumanne Sagini pamoja na mkewe Mariam Sagini kimetumika kwa ajili ya mahitaji ya wanafunzi na ukarabati wa miundombinu ya Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Chief Ihunyo Busegwe baada ya bweni moja kuteketea kwa moto.

Akizungumza na wahanga mara baada ya kutembelea na kukagua uhalibifu wa mali za wanafunzi pamoja na jengo la bweni lililopata ajali, Mbunge Sagini na mkewe wametoa msaada wa mafuta ya kujipaka, mashuka, sabuni, nguo za ndani, sare za shule, dawa za meno, kalamu, taulo za watoto wa kike, blanketi na ndoo za kuogea kwa wanafunzi 95 ambao ndio walipoteza mali zao kwa ajali ya moto.
Pia Mbunge Sagini amepokea na kutatua changamoto ya wanafunzi kuogea nje, hivyo ametoa kiasi cha shilingi 2,500,000/= kwajili ya ukarabati wa mabafu, na kumtaka mkandarasi kuhakikisha zoezi hilo linaenda kwa haraka zaidi ili wanafunzi waogee ndani.

Kwa upande wake Bi. Mariam Sagini ambaye ni mke wa Mbunge ametoa pole na kuwataka walimu waachane na kuomba msaada bali wafanye kazi yao ya kuwafundisha wanafunzi na kuwafariji, huku waliopewa dhamana ya uongozi ndio watashughulikia kuhakikisha mambo yote yanaenda sawa.
"Walimu fundisheni watoto wafaulu janga limetokea sisi ndio tutawajibika kuhakikisha hali inarudi kama awali, nimeguswa na mazingira wanayotumia kuogea wanafunzi natumaini Mh. Mbunge ameliona pia na amelitendea haki," amesema Mariam.

Pia Mkurugenzi wa Halmashauri ya Butiama Diana Sonno amewataka walimu wa shule zote kuboresha mahusiano na wanafunzi, kwani itasadia kupata taarifa mapema na kudhibiti viashiria ambavyo ni hatarishi na vyenye madhara makubwa mbeleni.
Naye Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Chief Ihunyo Muse Mwisawa ameeleza kuwa ajali hiyo ya moto ilitokea Tarehe 28, Januari mwaka huu Majira ya saa 1 usiku, baada ya wanafunzi wawili waliobaki kama waangalizi bweni kuona moshi mzito na kuanza kupiga kelele. Kwa kushirikiana na wanakijiji cha Busegwe walifanikiwa kuokoa nusu ya mali za wanafunzi na zingine zikiteketea.

Aidha Mwalimu Mwisawa amewashukuru mbunge na mkewe kwa msaada walioutoa pamoja na Viongozi mbalimbali walioambatana na mkurugenzi kwa kuendelea kutoa ushirikiano shuleni hapo, tangu siku ya kwanza kutokea kwa janga la moto.

No comments:

Powered by Blogger.