LIVE STREAM ADS

Header Ads

NHIF yatoa semina kwa viongozi wa vyama vya wafanyakazi Mwanza

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umekutana na viongozi wa vyama vya wafanyakazi Mkoa Mwanza kwa lengo la kuwajengea kuhusiana na shughuli mbalimbali zinazofanywa na mfuko huo katika kugharamia matibabu ya wanachama wake.

Meneja wa mfuko huo mkoani Mwanza, Jarlath Mushashu alisema hatua ya kuwajengea uelewa viongozi hao kuhusiana na huduma zinazotolewa na NHIF itawasaidia kufikisha elimu pia kwa wanachama wa vyama vyao na hivyo kuondoa malalamiko ambayo wakati mwingine hujitokeza.

Alisema kikao hicho ni sehemu ya utaratibu wa mfuko huo kukutana na wanachama wake na kutoa elimu kuhusiana na mabadiliko mbalimbali ya kisera na kiuendeshaji yanayofanywa na NHIF ikiwemo mabadiliko ya hivi karibuni ambayo yamewaondoa watoto wa wategemezi walio na zaidi ya umri wa miaka 18 kutoka kundi la watoto kwenda kundi la wanafunzi ikiwa bado wanasoma.

Akifungua kikao kazi hicho, Katibu Tawala Msaidizi Mkoa Mwanza, Tutubi John Magazeti alisema ipo haja kwa viongozi wa vyama vya wafanyakazi kuwahimiza wanachama wao kujiunga na mfuko wa NHIF kwani manufaa yake katika kugharamia matibabu ni makubwa na huondoa adha ambayo mtumishi anaweza kuipata pindi anapougua ikiwemo kushindwa kumudu gharama kubwa za matibabu.

"Mfuko huu umeboresha sana huduma zake, mimi ni mmoja wa wanufaika na ulinisaidia kugharamia matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando. Mfuko umekuwa ukilipia gharama kubwa za matibabu ikilinganishwa na michango tunayotoa" alisisitiza Magazeti.
Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
Meneja wa NHIF Mkoa Mwanza, Jarlath Mushashu akizungumza kwenye kikao kazi hicho/ semina.
Katibu Tawala Msaidizi Mkoa Mwanza anayeshughulikia Utawala, Tutubi Magazeti akifungua kikao hicho.
Baadhi ya washiriki wa kikao kazi hicho walishauri NHIF kuangalia upya suala la kuwaondoa watoto wa wategemezi walio na umri wa zaidi ya miaka 18 ili nao waendelee kunufaika badala ya kudhania kigezo wanaweza kujitegemea ikiwa si wanafunzi na hivyo kujiunga na vifurushi vingine vya mfuko huo.
Tazama BMG TV hapa chini

No comments:

Powered by Blogger.