LIVE STREAM ADS

Header Ads

Kiwanda cha Kusafisha Dhahabu Mwanza kuanza uzalishaji

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Shirika la Taifa la Madini (STAMICO), Dkt. Venance Mwasse amesema kiwanda cha kusafisha dhahabu jijini Mwanza (Mwanza Precious Metal Refinery) kinatarajiwa kuanza uzalishaji mwishoni mwa mwezi huu (Machi) baada ya shughuli ya kusimika mitambo kukamilika.

Dkt. Mwasse ameyasema hayo Machi 17, 2021 wakati akitoa taarifa ya ujenzi wa kiwanda hicho kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini inayoongozwa na Mwenyekiti wake, Dunstan Kitandula ilipofanya ziara kiwandani hapo.

Amesema hadi sasa gharama za ujenzi wa kiwanda hicho umefikia zaidi ya shilingi bilioni tisa za kitanzania na kitakuwa na uwezo wa kusafisha kilo 480 za dhahabu kwa siku na kuwa kiwanda cha tatau barani Afrika chenye uwezo wa kusafisha dhahabu hadi kufikia ubora wa asilimia 99.99.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dunstan Kitandula amesema wajumbe wameridhishwa na uwekezaji wa kiwanda hicho na kwamba wameshauri namna bora ya STAMICO na wabiya wake kukisimamia ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Naye Waziri wa Madini, Doto Biteko amesema wizara hiyo itafanyia kazi ushauri uliotolewa na wajumbe wa kamati hiyo ikiwemo kuweka mazingira rafiki kwa wachimbaji wadogo ili kunufaika na kiwanda hicho na kuleta manufaa kwa taifa.

Shirika la STAMICO kwa kushirikiana na mbiya wake kampuni ya Rozella General Trading kutoka nchini Dubai limekamilisha ujenzi wa kiwanda hicho na hivyo hatua itakayokuza soko la biashara ya madini nchini na kupunguza utoroshaji madini.
Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini wakiongozwa na Mwenyekiti wake, Dunstan Kitandula (wa kwanza kushoto) wakipata maelezo kuhusiana na uwekezaji uliofanywa kiwandani hapo.
Kiwanda cha kusafisha dhahabu jijini Mwanza (Mwanza Precious Metal Refinery) kimejengwa katika eneo la Sabasaba wilayani Ilemela jirani na kilipokuwa kiwanda cha ngozi Mwanza Tanarries.
Matarajio ni kuongeza mitambo kiwandani hapo katika awamu ijayo ili kiwe na uwezo wa kuzalisha kilo 960 za dhahabu kwa siku hatua itakayokifanya kuwa kiwanda cha pili barani Afrika kwa shughuli hiyo.
Tazama picha mbalimbali...
Tazama BMG TV hapa chini

No comments:

Powered by Blogger.