LIVE STREAM ADS

Header Ads

Vyombo vya habari Tanzania vyatakiwa kuwa na mkakati wa kujikwamua kifedha

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Na Ellukagha Kyusa, Mwanza
Waandishi wa Habari Tanzania wameeleza changamoto mbalimbali wanazo kumbana nazo katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku yanavyo athiriwa na ukosefu wa Uhuru wa Habari

Changamoto hizo zilielezwa kwenye mkutano uliofanyika kwa njia ya mtandao Mei 03, 2021 ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Habari Duniani na kuibua changamoto mbalimbali kwa Waandishi wa Habari.

Muwezeshaji Getrude John alisema kuwa waandishi wanawekewa vikwazo katika kuifikia jamii moja kwa moja na kuiomba mamlaka husika kufanya marekebisho ya sheria kandamizi katika vyombo vya habari.

Pia aliongeza kuwa waandishi wa habari na vyombo vya habari vimekumbwa na uhaba wa kifedha hivyo vinatakiwa kuwa na mkakati wa kujijengea uwezo wa kupata fedha ili kuwasaidia waajiriwa wao ambao ni waandishi wa habari kupata stahiki zao ili wafanye kazi kwa ufanisi.

Naye Mwezeshaji Jesse Kwayu ambaye pia ni Mjumbe wa Bodi ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) aliibua uwepo wa changamoto nyingi kwa waandishi wa habari ikiwemo suala la ukandamizwaji wa kupata taarifa kutoka kwenye mamlaka mbalimbali.

"Kumekuwa na sheria nyingi ambazo siyo rafiki kwenye tasnia ya habari zinazoleta hofu kwa waandishi kutafuta taarifa sahihi na kuzirusha kupitia vyombo vyao na hivyo kujikuta habari nyingi haziifikii jamii" alisema Kwayu.

Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olengurumwa alieleza kuwa waandishi wa habari wakikosa uhuru wa kutoa taarifa inaathiri jamii kwa kukosa haki ya kupata taarifa na kukosa mahali pa kupaza sauti zao na pia kuongeza kuwa vita dhidi ya kutetea haki za binadamu havitawezekana bila kuwepo vyombo vya habari na kuwasihi waandishi kuungana ili kuijenga tasnia ya habari na kutatua changamoto wanazo kutana nazo.

Maadhimisho ya mwaka huu ni maadhimisho ya 30 tangu kupitishwa kwa azimio la Windhoek nchini Namibia ambapo Mei 3 kila mwaka vyombo vya habari huadhimisha Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani.

Kongamano hilo liliandaliwa na Klabu ya Waandishi wa Habari ya Mkoa wa Mwanza kwa kushirikiana na Shirika la kimataifa la Internews na kuhudhuriwa na zaidi ya washiriki 60 kutoka mashirika na taasisi mbalimbali Tanzania.

No comments:

Powered by Blogger.