LIVE STREAM ADS

Header Ads

MWANZA "Wananchi wa Luchelele waiangukia Serikali"

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Wananchi wa Mtaa wa Luchelele jijini Mwanza wameiomba Serikali kuingilia kati suala lao la kurasimishiwa maeneo yao ili weweze kuyaendeleza na kufanya shughuli za kimaendeleo.

Wakizungumza na waandishi katika Ofisi za Halmashauri ya Jiji la Mwanza, wananchi hao waliokuwa wameenda kukutana na Mkurugenzi wa jiji hilo kama walivyokubaliana, walitoa kilio chao kwa Serikali kuingilia kati hili jambo hilo liweze kufikia mwisho.

Mmoja wa wananchi wa Luchelele ambaye ni mwakilishi wa wananchi wa eneo hilo, Fortunatus Maiga amesema mwaka 2014 ulifanyika upimaji kwa Sheria ya Mipango Miji kwa wananchi wote wa Kanda ya Luchelele ambapo mpango wa Halmashauri ya Jiji hilo ilikuwa kuwapa fedha chini ya kiwango ambapo fidia ilikuwa milioni tatu kwa kila hekali moja.

Maiga amesema wananchi walipinga hilo zoezi na wakafanya vikao ambapo 143 waliungana na kwenda mahakamani kupinga zoezi hilo ambapo wananchi wanakubaliana na upimaji lakini siyo kuondoka katika eneo hilo.

"Baada ya makubaliano hayo kabla ya wananchi kusaini, Mkurugenzi mwenyewe alikuja akasaini, Meya alisaini kwa niaba ya Baraza la Madiwani na Mwanasheria wao pia alisaini na sisi wawakilishi wa wananchi na Mwanasheria wetu tulisaini" amesema Maiga na kuongeza;

"Lakini utekelezaji umekuwa danadana baada ya Halmashauri kutotekeleza kwa wakati hivyo tunaiomba Serikali kupitia Rais, Waziri Mkuu na Waziri wa Ardhi kuitupia jicho la tatu na la kipekee halmashauri ya jiji la Mwanza" amesema Maiga.

Mwenyekiti wa Kamati ya wawakilishi wa wananchi wa Luchelele, Marlon Mbuya aliiomba Serikali kutatua suala hilo kwani limechukua muda mrefu takribani miaka 18 na kuchangia wananchi kutokufanya maendeleo.

Mwakilishi wa wananchi hao wa Luchelele, Nkeziah Kayamba alielezea kuwa baada ya kuzungumza na Mkuu wa Mkoa aliyepita, Mkurugenzi wa Jiji alisema angependa kuonana nao baada ya ugeni wa Rais kuondoka.

Kayamba amesema alimtafuta Mkurugenzi huyo na kumuomba miadi (appointment) ya kuonana naye ambapo ilikuwa siku ya Ijumaa wiki jailiyopita na aliongea nae akasema amtafute siku ya Jumanne (jana).

"Jana Jumanne kweli tulimtafuta akatuambia kwamba leo Jumatano Juni 23 mwaka huu, twende ofisini kwake saa mbili kamili asubuhi tuwe tumefika, kweli mimi na wenzangu tulikuja mapema sana kabla ya muda aliosema saa mbili kasoro tulikuwa tumefika, lakini cha kusikitisha ni kwamba mpaka sasa hivi saa tano hatujaonana naye" alisema Kayamba.

Alisema kuwa Mkurugenzi anataarifa zetu mara nyingi tunamsumbua PS ambaye angetuambia kuwa tusuburi au yupo kwenye kikao au kazi nyingine ila sasa hatujaonana nae na simu yake tumepiga haipatikani.

"Hali hiyo inatusikitisha, inatuathiri sana mfano mimi binafsi inaniathiri kama mtu ninayejitolea kuwasaidia wenzangu nina biashara zangu nashindwa kufanya shughuli zangu za kijamii kwa ajili ya jambo hili, sasa sisi tuliobeba mzigo tunashindwa je wenzetu wana hali gani, watu hawaendelezi maeneo yao hawezi kufanya biashara wala kujenga kwa sababu suala hilo halijafanyiwa utekelezaji" alieleza.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Jij hilo, Kiomoni Kibamba alipotafutwa na waandishi wa habari alikiri kulifahamu suala hilo na kueleza kuwa baada ya mwenge kupita Julai 7 mwaka huu atafika Luchelele kulishughulikia zaidi.

"Ninakikao cha maandalizi ya kupokea mwenge, nitakuja huko Julai 7 au 8" Amesema Kimbamba.

No comments:

Powered by Blogger.