LIVE STREAM ADS

Header Ads

Waziri Kalemani azindua mradi wa PERI URBAN wilayani Ilemela

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kamelani amezindua mradi wa kusambaza umeme awamu ya pili katika maeneo ya pembezoni mwa miji na majiji (Peri Urban) katika Wilaya Ilemela mkoani Mwanza ambao unaolenga kufikisha umeme katika mitaa yote ambayo haikuwa na nishati hiyo.

Hafla ya uzinduzi huo imefanyika Julai 09, 2021 katika Mtaa wa Ilalila, Kata ya Shibula wilayani humo ambapo wananchi katika mitaa 38 wanatarajiwa kuunganishiwa nishati ya umeme hadi kufikia Disemba 2022.

Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Kalemani amemtaka mkandarasi anayetekeleza mradi huo kampuni ya NAMIS Corporate kuhakikisha anafanya kazi usiku na mchana ili kuwaunganishia umeme wananchi katika mitaa hiyo.

“Ndani ya miezi 12 kuanzia sasa mitaa yote iwe imefikiwa na umeme, hatutarajii kuongeza muda, mkandarasi umekuwa ukifanya kazi nzuri lakini haina maana tusikushughulikie ukienda vibaya” amesisitiza Dkt. Kalemani.

Aidha Dkt. Kalemani ameagiza shirika la umeme TANESCO kufungua ofisi ndogo katika maeneo ya wananchi ili waweze kuchukua fomu na kulipia gharama za kuunganishiwa umeme ambazo ni shilingi elfu 27 tu badala ya wananchi kuwafuata ofisini.
“Wananchi tumieni umeme kwa ajili ya shughuli za kiuchumi ikiwemo kuanzisha viwanda vidogo kwani tutaweka transfoma 73 zenye uwezo wa KV 100 na KV 200 zenye uwezo wa kuwahudumia wawateja zaidi ya 250 ili kukidhi mahitaji ya watu wa mjini” ameeleza Dkt. Kalemani.

Naye Meneja wa REA Kanda ya Ziwa, Ernest Makale akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji REA amesema shilingi bilioni 9.94 zimetengwa kwa ajili ya kutekeleza mradi huo katika mitaa 59 mkoani Mwanza ambapo kwa Ilemela pekee zaidi ya bilioni sita zinatarajiwa kutumika kufikisha umeme katika mitaa 38 iliyokuwa imesalia.
Mradi wa Peri Urban unatekelezwa kwa majaribio katika majiji ya Mwanza, Arusha na Dodoma ikielezwa kuwa hadi kufikia Disemba 2022 changamoto ya ukosefu wa umeme katika maeneo ya mijini yatakiwa yametatuliwa.
Tazama BMG TV hapa chini

No comments:

Powered by Blogger.