LIVE STREAM ADS

Header Ads

Taasisi ya GST yatakiwa kutoa semina kwa wachimbaji madini Mwanza

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
WAZIRI wa Madini, Dkt. Doto Biteko ameitaka Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) kutoa semina kwa wachimbaji wadogo waliopo Mkoa wa Mwanza kuhusu mbinu za utafiti wa madini na namna bora ya kufanya uchenjuaji wa madini ili waweze kuongeza uzalishaji katika shughuli zao.

Dkt.Biteko ametoa agizo hilo Oktoba 11, 2021 alipokutana na kusikiliza changamoto za wachimbaji, wafanyabiasha pamoja na viongozi wa wachimbaji madini katika ziara yake aliyoifanya mkoani Mwanza.

Akijibu hoja ya Mbunge wa Jimbo la Sengerema, Khamis Tabasamu aliyewasilisha ombi ili STAMICO iende kusaidia shughuli za uchorongaji katika Wilaya ya Kwimba, Waziri Dkt. Biteko amemuagiza Kaimu Mkurugenzi wa STAMICO, Dkt.Venance Mwase kukamilisha utaratibu ili waende Kwimba wakafanye uchorongaji kama inavyofanyika mahali kwingine.

Wakati huo huo akizungumzia migogoro ya ardhi inayotokea kwa wachimbaji wa madini kuhusu umiliki wa ardhi, Dkt.Biteko amesema, haki ya madini na ardhi ni haki sawa zinazosimamiwa na Sheria ya Madini na Sheria ya Ardhi huku akisisitiza hakuna mwenye sheria ya juu kuliko mwenzake.

’’Hakuna mwenye ardhi, ardhi hii ni mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hakuna mwenye madini, madini haya ni mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,’’amesisitiza Dkt. Biteko.

Pia, Dkt.Biteko ameeleza kuwa, Serikali inakamilisha utaratibu wa kusajili viwanda vya kusafisha Dhahabu (Refinery) vilivyopo Mwanza, Geita na Dodoma.

Waziri Dkt.Biteko amesema, hadi sasa kuna viwanda vitatu vya kusafisha dhahabu vitakavyotumika kusafisha dhahabu kabla ya kusafirishwa nje ya nchi ili kuongeza thamani ya madini kabla ya kusafirishwa.

Aidha, Dkt.Biteko amefafanua kuwa, mpango wa Serikali ni kuona watanzania katika shughuli za uchimbaji madini wanafanya kazi zao kwa uhuru bila kuonewa, kunyanyaswa huku wakilipa kodi stahiki kwa maendeleo ya nchi.

Katika hatua nyingine, Dkt.Biteko amewataka Wafanyabiashara wa madini Mkoa wa Mwanza wenye ofisi katika jengo la Rock City Mall kuhamia katika soko jipya la madini lililopo katika eneo la Kiwanda cha Kusafisha Dhahabu cha Mwanza Precious Metals Limited.

Naye Naibu Waziri wa Ardhi, Dkt.Angelina Mabula amesema, kuanzishwa kwa kiwanda cha kisasa cha kusafisha dhahabu cha Mwanza Precious Metals kimesaidia kutoa ajira na kitakuza uchumi kwa wanachi wa Ilemela na Mwanza kwa ujumla.

Amesema, lengo la Serikali ni kuhakikisha inaondoa changamoto za wachimbaji wa kuanzisha kituo cha pamoja katika kiwanda hicho ili kutoa huduma zote kwa urahisi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Madini Mkoa wa Mwanza (MWAREMA), Richard Seni amesema kuwa, wachimbaji wadogo wameendelea kushiriki katika utoaji wa huduma mbalimbali za kijamii.

Aidha, amemuomba Waziri Dkt.Biteko kuzungumza na Sekta za Kibenki ili zikopeshe wachimbaji wadogo na wapate kinga ya kupata mikopo kwa shughuli mbalimbali za madini.

Kikao cha Waziri wa Madini, Dkt.Biteko kimehudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel, Mbunge wa Jimbo la Sengerema, Khamisi Tabasamu, Kaimu Mkurugenzi wa STAMICO, Dkt. Venance Mwase, Kamishina Msaidizi Francis Mihayo, Mkurugenzi wa Biashara na Ukaguzi wa Madini Tume ya Madini Venance Kasiki, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mwanza, Ernest Maganga, pamoja na wachimbaji, wafanyabiashara na viongozi wa wachimbaji wa madini wa Mkoa wa Mwanza.
Na Steven Nyamiti, WM
Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko Akizungumza na Wachimbaji, Wafanyabiashara na Viongozi wa Wachimbaji Madini pamoja na wadau mbalimbali wa Sekta ya Madini tarehe 11 Oktoba, 2021 Mkoani Mwanza.
Naibu Waziri wa Ardhi, Angelina Mabula Akizungumza na Wafanyabiashara wa madini pamoja na wadau mbalimbali wakati wa ziara ya Waziri wa Madini Dkt. Biteko Mkoani Mwanza.
Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji wa Madini Mkoa wa Mwanza (MWAREMA) Richard Seni akizungumza tarehe 11 Oktoba, 2021 Mkoani Mwanza.
Mbunge wa Jimbo la Sengerema Khamis Tabasamu akizungumza na Wachimbaji, Wafanyabiashara na Viongozi wa Wachimbaji wa madini.
Mfanyabiashara wa Madini akiwasilisha hoja kwa Waziri wa Madini Dkt Biteko wakati wa kikao cha wafanyabiashara na wachimbaji Mkoani Mwanza.
Tazama BMG TV hapa chini

No comments:

Powered by Blogger.