LIVE STREAM ADS

Header Ads

Profesa Asad afunguka umuhimu wa Katiba Mpya, kuondolewa kwenye nafasi ya CAG

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Aliyekuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Juma Asad amezungumzia sakata la kuondolewa kwenye nafasi hiyo mwaka 2019 na kubainisha kwamba hatua hiyo iligubikwa na maswali mengi kutoka kwa watu wa kada tofauti tofauti kwa kuwa anaamini aliondolewa kinyume na Katiba.

Profesa Asad ameyasema hayo jijini Dodoma wakati akizungumza kwenye mdahalo uliolenga kujadili kitabu cha mwandishi nguli wa habari, Jenerali Ulimwengu mada zikiwa ni miaka 25 ya Rai ya Jenerali, Demokrasia na Masuala yanayohusiana na Katiba nchini ulioandaliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) ambao uliwakutanisha wanazuoni kutoka vyuo mbalimbali, wabunge, viongozi wa Chama Cha wanasheria Tanganyika (TLS), Tume ya Haki za Bindamu na Utawala Bora ( THBUB) na Waadishi wa Habari.

Alisema anakerwa kuitwa CAG Mstaafu kwa sababu kuondolewa kwake kwenye nafasi hiyo kulienda kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 144 ambayo inaweka wazi sababu zitakazosababisha Kiongozi wa nafasi hiyo kuondolewa madarakani.
"Sababu hizo ni kama CAG atatimiza miaka 65 sasa mimi leo Oktoba 06, 2021 ndipo nimetimiza miaka 60, atashindwa kutekeleza majukumu yake kutokana na ugonjwa au sababu nyingine, utovu wa nidhamu na kwenda kinyume na maadili. Yote hayo mimi sikuyafanya naitwaje CAG Mstaafu? Huwa nakerwa sana na kauli hii" Alisema na kuongeza;

"Kuna umuhimu mkubwa wa kupata Katiba Mpya lakini ingawa hata hii tuliyonayo ya mwaka 1977 bado baadhi ya watawala hawaifuati kwa sababu wanaona wananchi hatuisimamii vizuri kutokana na kutishwa, Jenerali Ulimwengu ni hazina ya Taifa nampongeza sana kupitia makala zake alizoziandika tangu mwaka 1996 kama kuna jambo la kukosoa anakosoa anasimamia anachoamini.

"Wapo baadhi ya watu wamesoma lakini ni mazuzu hawatumii taaluma walizonazo wanalinda maslahi yao binafsi kwa kuwa wanatumia V8 na nyumba za Serikali, wanaogopa akitumia taaluma yake kusimamia ukweli akifukuzwa kazi atakosa hivyo vitu wakati anayetoa riziki ni Mungu, mimi nilisimamia ukweli na taaluma yangu ingawa sipo kwenye nafasi hiyo lakini bado napata riziki, ukweli ni kwamba mtu ambaye hana msimamo ni zuzu" alisisitiza Profesa Asad.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Wakili Anna Henga ambaye aliwakilishwa na Mratibu wake William Mtwazi alisema ili kujenga Tanzania ambayo kila mwananchi anaihitaji lazima kuwe na mifumo iliyoimara na thabiti ya kiutawala inayowajibika kwa wananchi wenyewe.

"Huwezi kuzungumzia mfumo imara wa kiutawala bila kuzungumzia Katiba ya nchi, ukisoma ibara ya nane ya katiba yetu utakubaliana na mimi kwamba wananchi ndiyo wenye mamlaka dhidi ya Serikali lakini wakati mwingine inaonekana ndivyo sivyo, wananchi tunamamlaka yaliyoandikwa kwenye katiba lakini inapokuja kwenye utekelezaji tunakuwa mashahidi kwenye sheria ambazo zimetungwa miaka michache iliyopita ambazo pamoja na mambo mengine zimelenga kupokonya uhuru wa wananchi katika kuamua au kutekeleza majukumu yao yanayolenga kujenga nchi au kuwajibisha mamlaka" alisema.

Alifafanua kwamba mdahalo huo ambao umewakutanisha washiriki kutoka mikoa ya Dodoma, Dar es Salaam, Iringa na Morogoro ni muhimu kwa sababu unatoa fursa ya kujadiliana, kushauriana na kuibua hoja ambazo zikijadiliwa zitasaidia kufikia maamuzi yenye tija kwa taifa.
Naye Jenerali Ulimwengu alisema kuna uhitaji wa Katiba Mpya itakayoendana na falsafa ya Taifa. Tanzania ni nchi pekee duniani ninayoijua ambayo imesema itakuwa na utawala wa kidemokrasia na itakuwa na wabunge wanaochaguliwa na wananchi lakini unaambiwa ukitaka kugombea nafasi yoyote lazima uwe mwanachama wa chama cha siasa.

"Kama si mwanachama wa chama cha siasa inamaana wewe ni nusu raia au robo raia huna uraia kamili mpaka ujibanze kwenye chama cha siasa suala hili tumelizungumza tangu mwaka 1992 hadi leo, hii inatoa tafsiri kwamba nguvu ya uhafidhina yaani nguvu ya kuturudisha nyuma ni kubwa zaidi kuliko nguvu ya kutupeleka mbele inayotambua umuhimu wa wananchi mmoja mmoja au katika makundi yao ambayo sio lazima yawe ya chama cha siasa inaweza kuwa jamii" alionya Ulimwengu.
Na Clara Matimo, Dodoma

No comments:

Powered by Blogger.