LIVE STREAM ADS

Header Ads

Mahitaji ya Umeme Kanda ya Ziwa yaongezeka, TANESCO wajipanga kutoa Huduma Bora

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Mahitaji ya wateja wapya wanaohitaji kuunganishiwa huduma ya nishati ya umeme katika mikoa ya Kanda ya Ziwa yameongezeka maradhufu kutoka maombi elfu sita hadi elfu 15 kwa mwezi ikielezwa kuwa sababu ni kushuka kwa gharama za kuunganishiwa huduma hiyo.

Meneja wa TANESO Kanda ya Ziwa, Mhandisi Henryfried Byabato aliyasema hayo Oktoba 07, 2021 wakati wa hafla fupi ya Wiki ya Huduma kwa Wateja iliyofanyika katika Ofisi za shirika hilo Igogo jijini Mwanza.

Mhandisi Byabato alisema miongoni mwa sababu zilizochochea ongezeko la maombi ya nishati ya umeme ni pamoja kushuka kwa gharama za kuunganishia huduma hiyo hadi shilingi elfu 27 ambapo aliwatoa hofu waliotuma maombi kuwa shirika hilo litawahudumia wote.
Alisema shirika hilo linalo jukumu kubwa la kuhakikisha linawaunganishia wateja wake wapiya nishati ya umeme huku likiendelea kuboresha huduma kwa ambao tayari wameunganishiwa ambapo alitumia fursa hiyo kutoa rai kwa wananchi kulinda miundombinu ya shirika hususani kutochoma moto maeneo nguzo zinapopita ili kuondoa adha ya kukatika kwa umeme.

Mhandisi Byabato alisema TANESCO ina umeme wa kutosha wa kuwahudumia wateja wake wakiwemo wateja wakubwa walio Kanda ya Ziwa kama vile mgodi wa North Mara, viwanda vya kusindika vinywaji kama Nyanza pamoja na wateja wapya ambao wanahitaji umeme mkubwa ambao ni pamoja na mradi wa SGR kipande cha kuanzia Isaka mkoani Shinyanga hadi Fela mkoani Mwanza.
Kwa upande wake Kaimu Meneja Tanesco Mkoa Mwanza, James Kabasa alisema shirika linawahudumia wateja 166,903 mkoani Mwanza na kwamba limejipanga ili kuhakikisha wateja wanapata huduma bora.
 
Naye Afisa Uhusiano TANESCO Mkoa Mwanza, Flaviana Moshi alisema Maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja yanaambatana na utoaji elimu ya usalama wa umeme kwa wateja wao kwa kuwafuata katika maeneo mbalimbali yenye mikusanyiko ikiwemo masokoni.
Mmoja wa wateja wa TANESCO jijini Mwanza, Dorothea Mgeta alisema baada ya gharama za kuunganishiwa umeme kupungua hadi elfu 27, wamepata fursa ya kuunganishiwa huduma hiyo kwani waliitamani muda mrefu huku Omary Khamis akitoa shime kwa shirika hilo kuongeza jitihada ili kuwaunganishia wateja wapya umeme kuendana na kasi ya maombi.

Mbali na kutoa elimu hiyo, wafanyakazi wa shirika wanatumia maadhimisho hayo kuimarisha mahusiano na wateja wao ambapo walipata fursa ya kula na kufurahia keki pamoja.

Wiki ya Huduma kwa Wateja huadhimishwa duniani kote kila mwaka kuanzia Oktoba 04-8 lengo likiwa ni kuwakumbusha watoa huduma wajibu wao ambapo kwa mwaka huu imeambatana na kaulimbiu ya "Nguvu ya Huduma" ikilenga kuchochea utoaji huduma bora kwa wateja ili kufikia mafanikio zaidi.

No comments:

Powered by Blogger.