LIVE STREAM ADS

Header Ads

DC Magu azindua Kampeni ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia 2021

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Mkuu wa Wilaya Magu mkoani Mwanza, Salum Kalli amezindua kampeni ya Siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia ambayo huadhimishwa kila mwaka kuanzia tarehe 25 Novemba hadi tarehe 10 Disemba kwa lengo la kuwaleta pamoja wadau mbalimbali kwa kushirikiana na Serikali kuhamasisha jamii kujiepusha na vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Uzinduzi wa kampeni hiyo umefanyika katika ukumbi wa WAMA wilayani Magu ikiratibiwa na Shirika la Kutetea Haki za Wanawake na Watoto KIVULINI lenye makazi yake Nyamhongolo jijini Mwanza ambalo limekuwa likitoa elimu ya kutokomeza ukatili wa kijinsia katika mikoa ya Kanda ya Ziwa ikewemo Magu mkoani Mwanza.

Akizungumza kwenye uzinduzi huo, Kalli amesema jamii haipaswi kunyamazia vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo vipigo kwa wanawake, kujihusisha kimapenzi na wanafunzi, mimba na ndoa za mapema.

Kalli ametumia fursa hiyo kuwahimiza waendesha bodaboda ambao ni miongoni mwa wadau waliohudhuria uzinduzi huo kujiepusha na mahusiano ya kimapenzi na wanafunzi wa kike kutokana na kudaiwa kwamba wamekuwa wakiwashawishi kuwapa lifti wakati wa kwenda ama kutosha shule ambapo amewasihi kuwa mabalozi wa kuwalinda wanafunzi hao.

"Mhe Rais Samia Suluhu Hassan ametuletea fedha shilingi bilioni 2.46 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba 123 vya madarasa katika Shule za Sekondari, tusipowalinda wanafunzi mnataka akasome nani kwenye hayo madarasa? Tushirikiane ili tuhakikishe wanatimiza ndoto zao" amesisitiza Kalli.
Katika hatua nyingine Kalli ameonya baadhi ya watendaji katika vyombo vya utoaji maamuzi kuchelewesha kesi zinazohusiana na vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo mimba kwa wanafunzi wa kike kwa kisingizio cha upelelezi kutokamilika na kusababisha kesi hizo kutopata mafanikio.

"Mwanafunzi anapewa ujauzito, anamtaja aliyempa huo ujauzito, mnamkamata lakini kesi haifiki mwisho hadi anajifungua na mtoto anaanza shule huku bado kesi haijasha kwa madai upelelezi haujakamilika, hapana" amekemea Kalli.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la KIVULINI, Yassin Ally amesema katika kuadhimisha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia 2021, shirika hilo litaendesha shughuli mbalimbali ikiwemo makongamano na midahalo ili kuendelea kuhamasisha jamii kupinga na kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Takwimu zilizotolewa na Jeshi la Polisi Mkoa Mwanza kitengo cha Dawati la Jinsia zimebainisha kuwa kesi 84 za ukatili wa kijinsia kwa mwaka 2020 zilipata mafanikio huku kesi 48 zikipata mafanikio kwa mwaka 2021 kuanzia mwezi Januari hadi Novemba na hatua za kisheria kuchukuliwa kwa wahusika.

Pia takwimu za jeshi la Polisi zilizochapishwa hivi karibuni kwenye tovuti ya Taifa ya Takwimu zinaonyesha kuwa katika kipindi cha kuanzia Mwezi Januari hadi Desemba 2020 kulikuwa makosa 11,001 ya ukatili wa kijinsia yaliyoripotiwa ikilinganishwa na makosa 12,223 yaliyoripotiwa mwaka 2019 ikiwa ni pungufu ya makosa 1,222.

Ufunguzi huo umeambatana na mdahalo uliowahusisha wanaharakati ngazi ya jamii, viongozi wa Halmashauri ya Magu, Jeshi la Polisi, Mahakama pamoja na bodaboda lengo likiwa kujengeana uelewa ili kwa pamoja wadau hao washirikiana kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia katika jamii.
Jumbe mbalimbali kwenye mdahalo wa ufunguzi wa kampeni ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia 2021 wilayani Magu.
"Kama Unapenda Sketi za Shule, Mshonee Mkeo"- KIVULINI.
Bango lenye kaulimbiu ya Kampeni ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia mwaka 2021.
Wanaharakati ngazi ya jamii wakifuatilia uzinduzi huo.
Mdahao ukiendelea ukumbini.
Mmoja wa bodaboda wilayani Magu akichangia mada kwenye mdahao wa uzinduzi wa Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia 2021 ambapo amesema watakuwa mstari wa mbele kupinga ukatili wa kijinisa katika jamii hususani kuwalinda wanafunzi wa kike.
Bodaboda ni usafiri salama.
"Chapa Kazi Siyo Mkeo"- KIVULINI.
Viongozi mbalimbali wilayani Magu wakijiandaa na uzinduzi wa kampeni ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia 2021 wilayani Magu.
Mkurugenzi wa Shirika la KIVULINI Yassin Ally (kushoto) akiteta jambo na Mkuu wa Wilaya Magu Salum Kalli (kulia) baada ya uzinduzi wa Kampeni ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia 2021.
Tazama BMG TV hapa chini

No comments:

Powered by Blogger.