LIVE STREAM ADS

Header Ads

Serikali yawakumbuka wafugaji

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (Mb) (aliiyeshikafimbo) akiswaga Ng'ombe kuelekea kwenye josho kwa ajili ya kuwaogesha katika Josho la Mekomariro lililopo Wilayani Bunda, mkoani Mara jana.Waziri Ndaki alikuwa Wilayani humo kukagua miundombinu ya Majosho ambapo aliwatakawafugaji kutunza miundombinu ya majosho ili kufanya uogeshaji wa Mifugo kuwa endelevu. Kulia kwake ( mwenye shati jeupe) ni Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Joshua Nassari.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (Mb) (kushoto) akizindua Josho la Sarakwa lilijengwa katika Kijiji cha Sarakwa Kilichopo Wilayani Bunda, Mkoani Mara. Josho hilo limejengwa kwa kiasi cha Shilingi Milioni 25 ambapo Serikali imetoa Sh. Milioni 18 na Wananchi wamechangia Sh.Milioni 7. Kulia ni Mbunge wa Jimbo la Bunda, Boniphace Getere.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki akizungumza na Wafugaji wa Kijiji cha Sarakwa muda mfupi baada ya kuzindua Josho la kuogeshea Mifugo lililojengwa katika kijiji hicho.
Pichani ni muonekano wa Josho jipya la Kisarakwa lililopo katika Kijiji cha Sarakwa, wilayani Bunda ambalo limezinduliwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (Mb).

Na Mbaraka Kambona, Mara
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amesema katika mwaka huu wa fedha 2021/2022 Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imepanga kujenga Majosho ya kuogeshea ng'ombe 178 nchi nzima ili kuiepusha mifugo na magonjwa yanayosababishwa na kupe na maradhi mengine yanayoambatana na kutokuogesha mifugo hiyo.

Waziri Ndaki ameyasema hayo katika ziara yake ya kukagua miundombinu ya majosho iliyopo katika Wilaya ya Bunda, mkoani Mara jana.

Akizungumza na wafugaji wanaofanya shughuli zao katika Vijiji vya Salamakati na Kisarakwa vilivyopo katika wilaya hiyo alisema lengo la Serikali ni kuweka josho kwenye kila kijiji kilicho na ng'ombe.

"Josho ni Zahanati ya Mifugo, hivyo sisi Wizara ya Mifugo na Uvuvi tunataka tuweke kila mahali ili wafugaji waweze kuogesha mifugo yao kuepukana na Kupe na magonjwa mengine yanayotokana na kutokuogesha mifugo" alisema.

Aliongeza kuwa mipango iliyopo ni kuendelea kuifanya mifugo iwe na afya njema jambo ambalo litasaidia kuongeza tija katika ufugaji ikiwemo kuuza mifugo hiyo kwa bei nzuri.

Aidha Waziri Ndaki aliwataka wafugaji hao na Wananchi kwa ujumla kuendelea kutunza miundo mbinu ya majosho iliyopo katika maeneo yao na ile itakayojengwa kwa sababu kwa kufanya hivyo kutasaidia uogeshaji wa mifugo kuwa endelevu.

Mbunge wa Bunda, Boniphace Getere alimuomba Mhe. Waziri Ndaki kuhamishia hela za ujenzi wa majosho katika Halmashauri ili iwe rahisi kuzifuatilia tofauti na ilivyo sasa ambapo hela za ujenzi zinatoka Wizarani jambo ambalo linaleta ugumu katika ufuatiliaji wake na hivyo kupelekea miradi ya ujenzi wa majosho kuchelewa kumalizika.

No comments:

Powered by Blogger.