LIVE STREAM ADS

Header Ads

Waziri Biteko ashuhudia makubaliano baina ya STAMICO na CRDB

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Ikiwa ni mwanzoni kabisa mwa mwaka 2022, Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko ameshuhudia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) pamoja na Benki ya CRDB wakitiliana saini Makubaliano ya Awali ya Kuwasaidia Wachimbaji Wadogo Kupata Mikopo.

Tukio hilo limefanyika wakati wa Mkutano Mkuu wa 24 wa Chama cha Wachimbaji Wanawake Tanzania (TAWOMA) uliofanyika jijini Dodoma Januari 24, 2022.

Akizungumza wakati akifungua Mkutano huo, Waziri wa Madini Dkt. Biteko alizipongeza taasisi hizo STAMICO na Benki ya CRDB zikiwemo taasisi nyingine za fedha kwa kubadilisha mtazamo dhidi ya wachimbaji wadogo na kuamua kuwakopesha.
Alisema STAMICO ina jukumu kubwa la kuthibitisha taarifa za jiolojia za wachimbaji wadogo kwa kuwa daraja kwa wachimbaji wadogo katika kupata mikopo kutoka katika taasisi za fedha.

Alitumia nafasi hiyo kuwapongeza wanachama wa TAWOMA na kuwataka kuwa vinara katika sekta ya madini ili kuondoa dhana ya unyonge wanapokuwa katika kazi zao katika mnyororo wa uchimbaji madini.

Alisema wanawake ni hazina kubwa kwa Taifa kwa kuwa wana uwezo wa kufanya kazi zaidi ya moja kwa wakati mmoja, wana kiwango kikubwa cha uaminifu na kwamba wanawake wakishirikishwa vizuri katika mnyororo wa uchimbaji madini itainufaisha jamii nzima ya Watanzania.
Aliwataka wanawake hao kutosahau jukumu lao la malezi kwa familia zao wakati wanatekeleza shughuli za uchimbaji ili kuweza kujenga jamii yenye tabia nzuri na kukubalika katika jamii. Pia, amewataka kukemea tabia ya kulalamika na badala yake kuwajenga katika kujituma na kujisimamia.

Akizungumza kama mlezi wa wachimbaji wadogo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Dkt. Venance Mwasse aliishukuru Benki ya CRDB kwa kukubali kuwasaidia Wachimbaji Wadogo kupata mikopo ambayo imekuwa kilio kikubwa cha muda mrefu kwa Wachimbaji Wadogo.

Alitoa pongezi kwa wanawake wachimbaji (TAWOMA) na kuwekeza kuwa wana nguvu ya uthubutu, ubunifu na ujasiri wa kujikita katika sekta hiyo ya uchimbaji mdogo ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikiaminika ni maalum kwa ajili ya wanaume tu.

No comments:

Powered by Blogger.