LIVE STREAM ADS

Header Ads

MWANZA: Benki TCB yakabidhi Milioni 15 kwa familia za Wanahabari waliofariki kwenye ajali

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi (wapili kulia) akikabidhi hundi ya shilingi milioni 15 kwa familia za wanahabari wa Mkoa Mwanza waliofariki kwa ajali iliyotokea Januari 11, 2022 eneo la Busega Simiyu wakielekea Ukerewe kikazi.
***

Benki ya Biashara ya Tanzania (Tanzania Commercial Bank- TCB PLC) imekabidhi hundi ya Shilingi Milion 15 kama mkono wa pole kwa familia za waandishi wa habari waliopoteza maisha kwenye ajali ya gari wakielekea ziarani Ukerewe, Januari 11, 2022.

Hafla ya kukabidhi hundi hio imefanyika Jumatatu Februari 21, 2022 katika ukumbi wa Mwanza Hotel jijini Mwanza ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya Nyamagana, Amina Makilagi.

Familia zilizopokea hundi hiyo ni za waandishi watatu ambao ni Anthony Chuwa, Johari Shani na Husna Mlanzi ambao enzi za uhai wao walikuwa wanachama wa kikundi cha Wanahabari Bima chenye lengo la kunufaika na bima ya majanga kupitia kampuni ya Alliance Life Insurance ambayo ni mshirika mwenza na benki ya TCB.

Akikabidhi hundi hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Amina Makilagi amewapongeza baadhi ya waandishi wa habari waliojiunga na kikundi cha Wanahabari Bima huku akiwataka ambao bado hawajajiunga wajiunge ili wapate msaada pindi majanga yanapowakumba.

Amesema kuwa kitendo cha waandishi wa habari kuamua kujinyima na kuanza kuwekeza kwenye Benki hiyo ni cha uzalendo ambacho kimewafuta machozi wanafamilia za marehemu.

Makilagi amewaasa waandishi ambao tayari wamejiunga na bima hiyo kuendelea kushirikiana na kupendana ili umoja huo uzidi kuimarika na kuwa chachu kwa wengine.

Aidha ametoa ushauri kwa Benki hiyo kuanzisha vifurushi vingine vipya vya kuwasaidia waandishi kikiwemo cha ada ili mwanachama anaposhindwa kumlipia ada mtoto wake kwa wakati, benki iweze kumsaidia kutokana na kile alichowekeza.

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Bima kutoka Tanzania Commercial Bank (TCB), Francis Kaaya amesema kuwa wamefanikiwa kutoa hundi hiyo kwa kushirikiana na kampuni ya Alliance Life Ansurance ambao wamekuwa wakilipa mafao hayo kwa wakati.

Naye Afisa Mauzo na Masoko kutoka Alliance Life Insurance, Jawa Masomo amesema kuwa wamekuwa wakilipa mafao kwa wakati ili yaweze kuwasaidia wafiwa katika kutatua shida za hapa na pale.

Akizungumza kwa niaba ya wafiwa ambao walikuwepo katika makabidhiano hayo, baba mzazi wa Antony Chuwa amesema wamefarijika kutokana na umoja huo walioanzisha wanahabari kwani ni kitu ambacho kimewapa faraja wanafamilia kwani waliofariki wameacha watoto na wajane hivyo fedha hizo zitawasaidia.
Mkuu wa Kitengo cha Bima kutoka Benki ya TCB, Francis Kaaya.
Waandishi wa habari, viongozi wa dini na ndugu wa marehemu wakiwa katika maombi.
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi.

No comments:

Powered by Blogger.