LIVE STREAM ADS

Header Ads

Tume ya Kurekebisha Sheria yafanya Tathmini ya Utekelezaji wa Sheria mbalimbali

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya kurekebisha sheria Tanzania, Khalist Luanda akiwasilisha mada kuhusu maisha baada ya kustaafu katika Ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) Tawi la Mbeya katika baraza la wafanyakazi lililofanyika.
Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya kurekebisha sheria Tanzania, Bw. Luanda akieleza mikakati mbalimbali walijiowekea ili kufanikisha malengo ya Tume hiyo.
Wajumbe wa baraza la wafanyakazi wakifuatilia mawasilisho mabalimbali.
Dereva wa Tume hiyo, Wense Evadi akichangia mada.
Mchumi kutoka Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania, Bi Fatma Alawi akiwasilisha mada kuhusu mikakati ya miaka mitano inayohusu maendeleo ya Tume.


Na Bashiri Salum, Mbeya
Tume ya Kurekebisha sheria Tanzania, imefanya tathmini ya utekelezaji wa sheria katika sekta mbalimbali zikiwemo sheria ya adhabu mbadala, sheria ya sekta ya utalii, na Sheria ya mifugo na uvuvi lengo likiwa ni kubaini changamoto zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wake na kuzifanyia tathmini kama malengo yaliyokusudiwa wakati wa kutungwa kwa sheria hizo yamefikiwa.

Akifafanua katika kikao cha Baraza la wafanyakazi kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa BOT Tawi la Mbeya katika wasilisho lililotolewa katika kikao hicho, Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume Bwana Khalist Michael Luanda akabainisha kwamba tathimini hiyo imefanyika kwa kupitia sheria nyingi zinazotumika katika sekta mbalimbali ambapo Tume inatarajia kukamilisha taarifa nne (4) za tathmini ya utekelezaji wa sheria.

Aidha Kaimu Katibu Mtendaji huyo alieleza mikakati ya Tume katika kuimarisha mawasiliano kwa kutumia vyombo vya habari ili kuitangaza taasisi hiyo ambapo kwa sasa wanajipanga kuandaa na kurusha vipindi vya redio na runinga kwa lengo la kutoa elimu ya sheria kwa umma.

Hata hivyo Luanda amebainisha kwamba Tume ya Kurekebisha Sheria imejipanga kutoa elimu kupitia vyombo vya habari juu ya Ushiriki wa wananchi katika mchakato wa maboresho ya Sheria hapa nchini .

“Sheria nyingine ambazo Tume imetoa elimu ni Sheria ya Mtoto, Sheria za Ajira Tanzania, Sheria za Utatuzi wa Migogoro ya Ardhi na Haki za walaji” alisisitiza katibu Mtendaji Khalist Luanda.

Naye Mchumi wa Tume ya Kurekebisha Sheria, Fatma Saidi Alawi wakati wa wasilisho lake kuhusu mikakati ya miaka mitano ya Taasisi hiyo amesema kipindi cha Julai, 2021 hadi Februari, 2022, Tume imechambua hukumu hamsini (50) za Mahakama ya Rufaa ya Tanzania na kuzibainisha Kanuni za Kisheria (Legal principles) mbalimbali zilizotumika katika kufanya uamuzi.

Aidha Fatma ametoa wito kwa wadau mbalimbali wanaohitaji kutumia Kanuni hizo kutembelea tovuti ya Tume kwa ajili ya kurahisisha watumiaji kufuatilia maendeleo ya Sheria mbalimbali kupitia maamuzi ya Mahakama.

Akiendelea na wasilisho lake, Fatma akafafanua kwamba Katika kipindi cha Julai 2021 hadi Februari, 2022, Tume imeshiriki katika kutafsiri sheria 17 zinazosimamiwa na Wizara ya Katiba na Sheria kutoka lugha ya Kiingereza kwenda lugha ya Kiswahili.

Akimalizia wasilisho lake, Fatma anasema kwamba Tume imeandaa Miongozo ya usuluhishi wa migogoro ya ardhi katika Mabaraza ya Kata na Mabaraza ya Ardhi ya Vijiji.

Hata hivyo baraza la wafanyakazi limehitimishwa baada ya wajumbe kutumia siku mbili kujadili mambo mbalimbali ya kiutumishi pamoja na mikakati ya kuboresha uendeshaji wa taasisi hiyo.

No comments:

Powered by Blogger.