LIVE STREAM ADS

Header Ads

Waziri Gwajima awaonya wanaokwamisha mikopo ya Halmashauri

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima amezionya baadhi ya Halmashauri nchini ambazo hazitekelezi kwa haki zoezi la utoaji mikopo ya asilimia 10 kwa wanawake, vijana na wenye ulemavu.

Waziri Gwajima amesema zipo Halmashauri nchini zimegubikwa na manung’uniko kwenye utoaji wa mikopo hiyo na hivyo kukwamisha jitihada za Serikali kuwakwamua kiuchumi wananchi.

Ameyasema hayo Machi 05, 2022 wakati akifungua Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ngazi ya Mkoa Mwanza lililofanyika katika uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza.

“Tumesikia manung’uniko kwamba utoaji wa hizo fedha kwenye baadhi ya Halmashauri ni changamoto, watu wanazungushwa, wanapewa kwa kujuana, taarifa hazieleweki na takwimu hazijulikani” amesema Waziri Gwajima na kuongeza;

“Yaani Mhe. Samia Suluhu Hassan atengeneze Sera, wananchi wakatwe kodi, Halmashauri ikusanye, halafu akae mtu mmoja atengeneze utaratibu wa kupindua mambo zisifike kwa walengwa, tusianze kuonana wabaya maana Wizara imeundwa na ufuatiliaji wa Sera hiyo sasa utaimarika” ameonya Waziri Gwajima.

Katika hatua nyingine ameipongeza Halmashauri ya Jiji la Mwanza kwa kutoa mikopo ya shilingi bilioni 3.2 katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita kwa vikundi 1,068 vyenye wanufaika 6,408 wakiwemo wanawake na kuwasaidia kuboresha shughuli zao na kujitegemea kiuchumi.

Aidha amesema kuwa Wizara yake kwa kushirikiana na wadau mbalimbali itahakikisha walengwa wa mikopo inayotolewa na Halmashauri wanajengewa uwezo ili mikopo wanayopokea ilete tija badala ya kuitumia katika shughuli zisizokusudiwa ikiwemo wanawake kununua mavazi/ madera

Naye Mkuu wa Mkoa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel amewataka wanawake kujitambua, kujiamini na kunogesha mahusiano katika ndoa zao hatua itakayosaidia kuondokana na migogoro ya kifamilia ambayo huchocheo manyanyaso na vitendo vya ukatili wa kijinsia katika jamii.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kutetea Haki za Wanawake na Wasichana KIVULINI, Yassin Ally amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha Wizara ya Maendeleo Jamii ambayo itashughulia changamoto za kijinsia na kuongeza ufanisi katika kusimamia Sera na mipango mbalimbali ya Wizara.

Hata hivyo Yassin ametoa rai kwa Serikali kuweka mkakati ili kuwanusuru na ukatili watoto wadogo wanaobebwa kwenye mabasi ya shule kwani baadhi ya wasaidizi wa mabasi hayo wanatuhumiwa kuwafanyia ukatili wa kingono.

Kilele cha Siku ya Wanawake Duniani hufanyika kila kwaka Machi 08 ambapo mwaka huu kauli mbiu ni “Kizazi cha Haki na Usawa kwa Maendeleo Endelevu, Tujitokeze Kuhesabiwa”.
Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
Mkuu wa Mkoa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel akizungumza kwenye Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ngazi ya Mkoa Mwanza.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la KIVULINI, Yassin Ally akitoa salamu kwenye Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ngazi ya Mkoa Mwanza
Mchungaji Theresia Mkami akisoma Risala ya wanawake Mkoa Mwanza ambapo ametoa rai kwa wanaume kuwaamini na kuwawezesha wanawake katika shughuli za kiuchumi ili kuongeza pato la kaya huku akisema mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri imeleta tija kubwa katika jamii.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kutetea Haki za Wanawake na Wasichana KIVULINI, Yassin Ally (kushoto) akiwa kwenye maandamano wakati wa Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ngazi ya Mkoa Mwanza.
Wanafunzi wa kike jijini Mwanza wakiwa na mabango yenye jumbe mbalimbali za kupinga ukatili wa kijinsia.
Waendesha bodaboda wakiwa kwenye maandamano kuelekea kwenye Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ngazi ya Mkoa Mwanza.
Wanawake wakiwa kwenye maandamano yaliyoanzia eneo la 'Gandh Hall' kuelekea kwenye uwanja wa Nyamagana ulipofanyika ufunguzi wa Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani 2022 ngazi ya Mkoa Mwanza.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kutetea Haki za Wanawake na Wasichana KIVULINI, Yassin Ally (kulia) akiwa kwenye maandamano wakati wa Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ngazi ya Mkoa Mwanza.
Viongozi mbalimbali meza kuu wakisoma jumbe za mabango mbalimbali.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima (katikati) akipokea maandamano wakati wa Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ngazi ya Mkoa Mwanza.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima (katikati) akicheza wakati wa Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ngazi ya Mkoa Mwanza.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima (katikati) akicheza ngoma za asili wakati wa Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ngazi ya Mkoa Mwanza.
Watoto wenye ualibino wakitoa ujumbe wa kupinga ukatili wa kijinsia wakati wa Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ngazi ya Mkoa Mwanza.

No comments:

Powered by Blogger.