LIVE STREAM ADS

Header Ads

Raia wa kigeni 34 wanaswa kwa kuingia nchini kinyemela

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa linawashikiria watu 34 wanaodhaniwa kuwa ni wahamiaji haramu kutoka nchini Ethiopia wakisafirishwa kuelekea nchini Afrika Kusini baada ya kuwakamata katika eneo la Kitonga Wilaya ya Kilolo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, ACP Allan Bukumbi amesema kuwa wamefanikiwa kuwakamata watu hao kwa ushirikiano na Idara ya Uhamiaji mkoani Iringa.

ACP Bukumbi alisema kando ya kukamatwa kwa raia hao wa kigeni Jjshi la polisi linamshikiria dereva wa lori, Maulid Chinunga (37) mkazi wa Dar es salaam aliyehusika kuwasafirisha raia hao wakigeni kinyume na sheria.

Alisema kuwa tarehe 27/04/2022 majira ya Saa 10:00 jioni, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Jeshi la Uhamiaji Mkoa wa Iringa eneo la Comfort-Kitonga Kata na Tarafa ya Mahenge, Wilaya ya Kilolo Mkoa wa Iringa, tulifanikiwa kumkamata dereva Maulid Chinunga (37) mkazi wa Dar es salaam akiwa anasafirisha raia wa kigeni wapatao 34 kutoka nchini Ethiopia wakitokea mkoani Pwani kuelekea Tunduma mkoani Mbeya kwenye gari aina ya FAW yenye namba za usajili T. 529 DXF na tela T. 826 DXP mali ya kampuni Mighty Logistics LTD ambapo watafikishwa mahakamani upelelezi utakapokamilika.

Pia Kamanda Bukumbi alitaja uwepo wa tukio la mtu mmoja mkazi wa Kalenga Wilayani Iringa kukamatwa na meno ya tembo aliyoyaficha katika korongo.

Alisema kuwa mnamo tarehe 16/04/2022 majira ya Saa 10:20 jioni maeneo ya Bumila Kata ya Nzihi Tarafa ya Kalenga Mkoa wa Iringa, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na kikosi dhidi ya ujangiri (KDU) tulifanikiwa kumkamata Romanus Mututuri (45) akiwa na vipande viwili vya Meno ya Tembo yenye thamani ya Tsh, 35,189,122/= aliyokuwa ameyaficha kwenye korongo baada ya kupokea taarifa fiche kutoka mwananchi zilizowezesha kukamatwa kwake.

"Mwisho nitoe rai kwa wananchi wa Mkoa wa Iringa kuwa na utii wa sheria katika kipindi hiki tunapoelekea Sikukuu ya EID EL-FITR, wasiache nyumba zao bila uangalizi muda wote, watumiaji wa vyombo vya moto (magari, bajaji na pikipiki) njia kuu na maeneo mengine wawe na utii, pia wananchi waache kujihusisha na vitendo vya uhalifuna badala yake washirikiane na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa kwa wakati ili ziweze kushughulikiwa" alisema ACP Bukumbi.

No comments:

Powered by Blogger.