LIVE STREAM ADS

Header Ads

Mwenyekiti MPC ampongeza Waziri Nape kwa agizo lake

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com 
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Nnauye.
***

Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa Mwanza (MPC), Edwin Soko amempongeza Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Nnauye kwa kuagiza maafisa habari na mawasiliano serikalini kuhuisha tovuti za wizara na taasisi zao ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa.

Soko ametoa pongezi hizo wakati akizungumza kwenye maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani yaliyofanyika ngazi ya Mkoa Mwanza Mei 10, 2022 baada ya kupisha maadhimisho ya kitaifa yalitofanyika Mei 03, 2022 jijini Arusha.

“Waziri Nape akiwa Tanga kwenye mkutano wa maafisa habari na mawasiliano serikalini, alitoa muda wa siku 14 wahuishe taarifa kwenye tovuti na mitandao ya kijamii ya wizara na taasisi za Serikali, hii itawezesha pia waandishi wa habari kupata taarifa mbalimbali zitakazosaidia kutimiza vyema majukumu yao” alisema Soko.

Katika hatua nyingine Soko ametoa rai kwa viongozi wa umma kutoa ushirikiano kwa waandishi wa habari kwa kutominya upatikanaji wa taarifa hatua itakayosaidia hatua stahiki kuchukuliwa kwa yale yanayoibuliwa na waandishi wa habari ikiwemo kwenye utekelezaji wa miadi ya maendeleo.

Pia Soko amewakumbusha waandishi wa habari kuzingati misingi ya taaluma ya habari wakikosoa na kutoa suluhisho kwenye changamoto mbalimbali wanazoziibua akisema “tufanye kazi kwa kuzingatia uzalendo na misingi ya habari kwani nchi hii ni yetu sote na tunapaswa kuijenga pamoja”.

Naye Mratibu wa Program kutoka Shirika la Internews Tanzania, Shaban Maganga amesema shirika hilo limekuwa likisaidia vyombo vya habari na waandishi wa habari kufanya kazi kwa ufanisi pamoja na kuhimiza mabadiliko ya sheria zinazolalamikiwa na waandishi wa habari.

Awali akifungua maadhimisho hayo, Mkuu wa Wilaya ya Magu Salum Kalli amewahimiza waandishi wa habari kutimiza majukumu yao kwa kuzingatia weledi huku wakihakikisha wanatoa habari sahihi kwa manufaa ya jamii.

Hata hivyo baadhi ya waandishi wa habari walioshiriki maadhimisho hayo, licha ya kupongeza mazingira rafiki ya ufanyaji kazi kutokana na hamasa anayoitoa Rais Samia Suluhu Hassan, bado wanahofu juu ya sheria tata zilizopo hivyo ni kiu yao kuona zinafanyiwa marekebisho mapema.

Maadhimisho hayo yameandaliwa na MPC kwa kushirikiana na shirika la Internew Tanzania ambapo pamoja na mambo mengine, pia waandishi wa habari wamejengewa uwezo kuhusu mada mbalimbali ikiwemo usalama mtandaoni, Uhuru wa Kujieleza mtandaoni pamoja na Uhuru wa Vyombo vya Habari ambapo wamekumbushwa sheria na kanuni za kuwaweka salama.
Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
Mwenyekiti wa MPC, Edwin Soko akizungumza kwenye maadhimisho hayo.
Mratibu wa Programu kutoka Shirika la Internews Tanzania, Shaban Maganga akizungumza kwenye maadhimisho hayo.
Mkuu wa Wilaya Magu, Salum Kalli akifungua maadhimisho hayo.
Washiriki wakifuatilia mada kutoka kwa Mwenyekiti wa MPC, Edwin Soko (kulia).
Mkufunzi Lucyphine Kilanga akiwasilisha mada kuhusu usalama mtandaoni.
Mkufunzi Deus Nugaywa akiwasilisha mada kuhudu Uhuru wa Vyombo vya Habari Tanzania.
Picha ya pamoja.

No comments:

Powered by Blogger.