LIVE STREAM ADS

Header Ads

Watanzania wahimizwa kuchangamkia fursa katika Sekta ya Madini

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adolf Ndunguru tarehe 22 Mei, 2022 amefunga Jukwaa la Kwanza la Utekelezaji wa Ushirikishwaji wa Watanzania Katika Sekta ya Madini lililoanza tangu tarehe 20 Mei 2022 jijini Mwanza.

Jukwaa hilo lililoambatana na maonesho lilishirikisha wadau wa madini wakiwa ni pamoja na wachimbaji wa madini, watoa huduma kwenye shughuli za uchimbaji wa madini, mabenki na watendaji kutoka taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Madini.

Akizungumza kwenye ufungaji wa jukwaa hilo Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adolf Ndunguru amesema kuwa Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini imeandaa jukwaa hilo kwa lengo la kuhakikisha watanzania wanabaini fursa zilizopo na kushiriki kikamilifu kwenye Sekta ya Madini.

Amesema kuwa Wizara ya Madini itaendelea kuhakikisha watanzania wananufaika na fursa zitokanazo na Sekta ya Madini kupitia ushirikishwaji wa watanzania katika utoaji huduma mbalimbali huku pia ikiendelea kutatua changamoto mbalimbali katika sekta hiyo.

Aidha amewataka wadau wa madini kushiriki katika zoezi la sensa linalotarajiwa kufanyika mwezi Agosti mwaka huu ili kuiwezesha Serikali kuweka mipango mbalimbali ya maendeleo.

Wakati huohuo, Ndunguru ametoa tuzo na vyeti kwa wadhamini wa Jukwaa hilo wakiwa ni pamoja na Equity Bank (Tanzania) Limited, CMS (Tanzania) Limited, Twiga Minerals Corporation Limited na BR Drilling Limited.
Wengine ni pamoja na Tansec Limited, Boart Longyear (Tanzania) Limited, Geita Gold Mining Limited, Williamson Diamonds Limited, Tembo Nickel Corporation Limited, BG Umoja Services Limited, Epsom Limited, African Assay Laboratories, Tanga Cement Limited, Shanta Mining Co. Limited na SGA Guards Tanzania Limited.
Akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi Kamishna wa Tume ya Madini, Janeth Reuben Lekashingo sambamba na kushukuru kwa ushirikiano mkubwa unaotolewa na Wizara ya Madini kwenye usimamizi wa Sekta ya Madini amewataka wananchi kuchangamkia fursa zilizopo kwenye Sekta ya Madini.
Naye Kamishna wa Madini, Dkt. Abdulrahman Mwanga amesema kuwa jukwaa limewapa mwanga wadau wengi wa madini kuhusu dhana nzima ya ushirikishwaji wa watanzania katika Sekta ya Madini.

Aidha amesema kuwa jukwaa hilo limetumika kama njia mojawapo ya kujadili namna ya kuzitatua changamoto mbalimbali zinazoikumba Sekta ya Madini hususan kwenye eneo la ushirikishwaji wa watanzania katika Sekta ya Madini.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Kanali Dennis Mwila akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel ameipongeza Tume ya Madini kwa kuandaa jukwaa la kizalendo lenye lengo la kuhakikisha watanzania wanafahamu namna wanavyoweza kushiriki kwenye Sekta ya madini kupitia utoaji wa huduma kwenye migodi ya madini.

Aidha amewataka washiriki wa jukwaa hilo kuwa wazalendo kwenye utekelezaji wa shughuli zao na kupata fursa zaidi kwenye migodi ya madini.
Katibu Mtendaji Tume ya Madini, Yahya Samamba akizungumza wakati kilele cha jukwaa hilo.
Baadhi ya watumishi wa Tume ya Madini wakifuatilia jukwaa hilo.
Watumishi Tume ya Madini.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adolf Ndunguru akipata maelezo baada ya kutembelea maonesho ya wadau wa seka ya madini walioshiriki jukwaa hilo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adolf Ndunguru (wa tano kushoto) akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi mbalimbali.

No comments:

Powered by Blogger.