LIVE STREAM ADS

Header Ads

Shirika la EMEDO laahidi kushirikiana na wanahabari "tuna miradi mingi"

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Mkurugenzi Mtendaji Shirika la usimamizi wa mazingira na utunzaji rasilimali za uvuvi EMEDO, Editrudith Lukanga akizungumza kwenye hafla ya Usiku wa Waandishi na Wadau wa Habari Kanda ya Ziwa. Shirika hilo lenye makazi yake jijini Mwanza pia linatekeleza mradi wa kupunguza vifo vya wavuvi katika Ziwa Victoria.
***
Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la usimamizi wa mazingira na utunzania wa rasilimali za uvuvi (EMEDO), Editrudith Lukanga amesisitiza kuwa shirika hilo litaendelea kufanya kazi kwa ukaribu na waandishi wa habari kwani ni wadau muhimu katika kufikisha ujumbe kwa jamii.

Lukanga aliyasema hayo Juni 03, 2022 wakati akitoa salamu za shirika lake kwenye hafla ya Usiku wa Waandishi na Wadau wa Habari Kanda ya Ziwa iliyofanyika Rock City Mall jijini Mwanza uliondaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa Mwanza (MPC).

Aliwapongeza waandishi wa habari mkoani Mwanza kupitia umoja wao wa MPC kwa kuandaa hafla hiyo na kuongeza kuwa waandishi wa habari wana nafasi kubwa katika kufikisha taarifa kwa wananchi ambapo tukio linaweza kusambaa dunia nzima kwa muda mfupi hivyo ni vyema wakatambua umuhimu wao na kufanya kazi zinazogusa jamii.

"Tunathamini mchango wenu katika kuhabarisha na kuelimisha, nafasi yenu ni kubwa kwani jambo linaweza kutokea hapa na kusambaa kwa muda mfupi ulimwengu mzima hivyo muone jinsi mlivyo na nafasi kubwa" alisema Lukanga na kuongeza;

"Tuko tayari kufanya kazi nanyi, tuna miradi mingi inayogusa moja kwa moja jamii hivyo niwaombe tuendelee kushirikina msije mkaangalia matukio makubwa tu kwani mnapofanya kazi kwenye jamii mnagusa watu wengi" alisema Lukanga.

Lukanga alitumia fursa hiyo pia kuwakaribisha wadau mbalimbali wakiwemo waandishi wa habari katika kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani itakayofanyika Juni 05, 2022 itakayoambatana na shughuli mbalimbali ikiweno kufanya usafi.

Katika hafla hiyo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Mkoa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel ambaye aliwahimiza waamiliki wa vyombo vya habari na taasisi mbalimbali kuboresha maslahi ya waandishi wa habari ili kuendana na gharama za maisha lakini pia kama ambavyo watumishi wengine wakiwemo wa Serikali walivyoongezewa mshahara kwa asilimia 23.3.

Mhandisi Gabriel alihimiza mpango wa kuwakopesha viwanja waandishi wa habari mkoani Mwanza kuwa na masharti nafuu ili wengine wanufaike na mpango huo ulioandaliwa na MPC kwa kushirikiana na benki ya Mkombozi pamoja na kampuni yabMwanza Makazi Developers.

Aliwaomba waandishi wa habari kuendelea kuelimisha wananchi kutambua umuhimu wa zoezi la Sensa ya Watu na Makazi linalotarajiwa kufanyika Oktoba 23, 2022, kuendelea kuchukua tahadhari ya ugonjwa wa UVIKO 19, kupata chanjo ya ugonjwa huo kwani bado upo huku akiahidi kushirikiana na MPC kufanikisha ujenzi wa ofisi ambapo katika hafla hiyo alizindua akaunti maalum ya benki kwa ajili ya wadau kuanza kuchangia gharama za ujenzi.

Katika hatua nyingine Mhandisi Gabriel alikemea tabia ya ukatili wa kijinsia kwenye ndoa ikiwemo mauaji yaliyoripotiwa kutokea hivi karibuni jijini Mwanza na kuwahimiza waandishi kutumia kalamu zao kuelimisha umma, kufichua matukio hayo kabla hayajatokea na pale dalili za kutishia kuua zinapotea, watoe taarifa na Serikali itachukua hatua mara moja ikiwemo kuwapokonya silaha wanaotishia.

"Mke hapigwi na silaha, anapigwa na doti ya kanga mpya au busu, ukiona unapigwa na ngumi, ujue hali imebadilika unahitaji msaada wa Serikali, mme akikasirika anapaswa akupige na laki tano au milioni, anakuambia mwanamke acha ukorofi, Mungu akubariki upate mme anayekupiga kwa hela na siyo makofi" alisema Mhandisi Gabriel.

Awali Mwenyekiti wa MPC, Edwin Soko alisema hafla ya Usiku wa Waandishi na Wadau wa Habari Kanda ya Ziwa ambayo imefanyika mwaka wa tatu mwaka huu inalenga kuimarisha mahusiano, wadau kuoata fursa ya kuelesha shughuli wanazozifanya na kwamba mkakati uliopo ni mwakani kufanyika kitaifa ili kuwaleta pamoja wadau wengi zaidi.

Soko aliwaomba wadau kuchangia ujenzi wa ofisi ya waandishi wa habari mkoani Mwanza kwenye kiwanja chao kilichopo Kisesa ili kuondokana na kutumia gharama kubwa kwenye jengo la kupanga lakini pia kupanua wigo wa ofisi ikiwemo kujenga studio itakayotumika kuwajengea ujuzi waandishi wa habari ili kutekeleza majukumu yao kwa welezi zaidi.

Miongoni mwa wadau waliofanikisha hafla hiyo ni pamoja na kampuni ya TBL, TCRA, NSSF, Jambo Food Product, UTPC, Metro FM, Clouds Media Group, TRA, TIRA, EMEDO, YUHOMA Education Link, Kampuni ya Huduma za Meli MSCL, Rahara Media/ RFA, Cecy Toto & Gift Shop pamoja na SBC/ Pepsi.
Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa Mwanza (MPC), Edwin Soko akizungumza kwenye hafla ya Usiku wa Waandishi na Wadau wa Habari Kanda ya Ziwa.
Meneja wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Kanda ya Ziwa, Mhandisi Francis Mihayo akitoa salamu kwenye hafla hiyo ambapo aliahidi mamlaka hiyo kwa kushirikiana na ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mwanza kuwasaidia waandishi wa habari kupata stahiki zao.
Mkuu wa Mkoa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel akizungumza kwenye hafla hiyo.
Mkuu wa Mkoa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel (kulia) akimkabidhi cheti cha shukurani Mkurugenzi Mtendaji Shirika la EMEDO, Editrudith Lukanga (kushoto) kwa kusaidia kufanikisha hafla ya Usiku wa Waandishi na Wadau wa Habari Kanda ya Ziwa.
Mkuu wa Mkoa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel (kulia) akimkabidhi cheti cha shukurani Meneja wa Redio Metro FM, Alex Ngusa (kushoto) kwa kusaidia kufanikisha hafla ya Usiku wa Waandishi na Wadau wa Habari Kanda ya Ziwa.
Mkuu wa Mkoa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel (kushoto) akizinda akaunti maalumu kwa ajili ya wadau kuchangia ujenzi wa ofisi ya Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa Mwanza (MPC).
Mkuu wa Mkoa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel (kushoto) na Mwenyekiti wa MPC, Edwin Soko (kulia) wakionyesha akaunti maalum ya chama cha waandishi wa habari mkoani Mwanza (MPC) kwa ajili ya wadau kuchangia ujenzi wa ofisi ya chama hicho.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la EMEDO, Edtrudith Lukanga (kushoto) akiwasilisha mchango wa fedha kwa ajili ya kuchangia ujenzi wa ofisi za MPC.
Mkuu wa Mkoa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel (kushoto) akimkabidhi Katibu wa MPC, Blandina Alistides (kulia) kiasi cha fedha kilichotolewa na wadau kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya MPC.
Mkuu wa Mkoa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel (kulia), wadau na waandishi wa habari wakiwa kwenye hafla hiyo.

No comments:

Powered by Blogger.