LIVE STREAM ADS

Header Ads

Watumishi Wizara ya Maji watakiwa kufanya kazi kwa weledi

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (wa pili kulia) akiwasikiliza watumishi Sekta ya Maji Mkoani Katavi (hawapo pichani).
Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira, Mhandisi Mwajuma Waziri akizungumza na watumishi Sekta ya Maji Mkoani Rukwa (hawapo pichani). Wa pili kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga.
Baadhi ya watumishi kutoka Ofisi za RUWASA Mkoa wa Katavi na Mamlaka ya Maji Mpanda wakimsikiliza Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (hayupo pichani).
Baadhi ya watumishi wa Sekta ya Maji Mkoani Rukwa wakimsikiliza Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (hayupo pichani).
Baadhi ya watumishi wa Sekta ya Maji Mkoani Songwe wakimsikiliza Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (hayupo pichani).
***


Na Mohamed Saif
Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga amewaasa watumishi wote katika Sekta ya Maji kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, taratibu na kanuni ili kufikia malengo ya kuwafikishia wananchi huduma toshelevu ya majisafi na salama.

Katibu Mkuu Sanga ametoa maelekezo hayo kwa nyakati tofauti alipokutana na watumishi wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maji katika Mikoa ya Katavi, Rukwa na Songwe.

“Sisi sote hapa ni watumishi wa umma; tunazo sheria, taratibu na kanuni za kiutumishi zinazotuongoza, ni muhimu kila mmojawetu akatimiza majukumu yake kwa kuzingatia haya mambo matatu” alisisitiza Katibu Mkuu Sanga.

Mhandisi Sanga aliwaelekeza watumishi wote kwenye Sekta ya Maji kuepuka kuwa kero kwa wananchi na badala yake wawe ni wafumbuzi wa kero zinazowakabili wananchi hasa ikizingatiwa kwamba huduma ya maji haina mbadala na kwamba kila mwananchi anayo haki ya kupatiwa huduma bila kikwazo.

Aliwaasa watumishi hao kupenda kazi zao, kushirikiana, kuthaminiana, kupendana, kuheshimiana na kutambua jukumu la kila mmoja kwa jamii anayoihudumia ili kuepusha migongano isiyo ya lazima.

Alisema mwananchi anachohitaji ni kupata huduma ya maji haijalishi huduma hiyo anaipata kutoka kwenye Mamlaka ya Maji ama RUWASA na hivyo alizielekeza taasisi zote zilizo chini ya Wizara ya Maji kushirikiana hasa ikizingatiwa jukumu la msingi la taasisi hizo ni kuhakikisha mwananchi anapata huduma toshelevu ya majisafi na salama.

“Wananchi wanatutegemea kuwafikishia huduma bora, toshelevu na ya uhakika, tusiwe kikwazo katika hili. Kila mmoja kwa nafasi alionayo na kwa taasisi aliyopo amsaidie mwenzake kufikia lengo hili na asiwe kikwazo kwa mwenzake” alielekeza Mhandisi Sanga.

Aidha, watumishi hao walieleza changamoto zinazowakabili ili kuzipatia ufumbuzi na pia walipata fursa ya kuzungumza na Mhe. Jumaa Aweso, Waziri wa Maji kwa njia ya simu kupitia Mhandisi Sanga na kupata nasaha zake.

Walipongeza utaratibu huo wa Katibu Mkuu Sanga wa kuwatembelea na kujadiliana kwa pamoja kuhusu utekelezaji wa majukumu yao na ufumbuzi wa pamoja wa changamoto na kero mbalimbali zinazowakabili.

“Tunakushukuru sana Katibu Mkuu kwa utaratibu huu unaoendelea nao, tumepata nafasi ya kukueleza ana kwa ana masuala mbalimbali ya kiutendaji na tumefarijika kupata nasaha zako na za Mhe. Waziri ambazo zinaleta motisha kwenye utendaji wetu,” alisema Ligo Gambi, Fundi Sanifu Mamlaka ya Majisafi Mpanda (MUWASA).

Akizungumza kwa nyakati tofauti katika vikao hivyo, Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri ambaye aliambatana na Katibu Mkuu Sanga aliwaelekeza watumishi kuwa na maadili ya kazi, wajitume na wachape kazi kwa bidii ili kuleta matokeo chanya.

Katibu Mkuu Sanga amefanya ziara kwenye mikoa hiyo ili kujionea utekelezwaji wa miradi unaoendelea, kuzungumza na watumishi na kukagua uwezekano wa kujenga miradi mikubwa kwenye maeneo yenye vyanzo toshelevu vya maji.

Vikao hivyo vya Katibu Mkuu Wizara ya Maji na watumishi maarufu kama ‘zungumza na Katibu Mkuu’ vinavyotoa fursa kwa watumishi kumueleza Katibu Mkuu na Menejimenti yake ya Wizara ya Maji jambo lolote linalowatatiza katika utendaji wa majukumu yao ili kupata ufumbuzi.

No comments:

Powered by Blogger.