LIVE STREAM ADS

Header Ads

Wananchi Songwe kupata mradi mkubwa wa maji

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (kulia) alipowasili katika Kijiji cha Bupigu Wilaya ya Ileje kukagua uwezekano wa kuwa na mradi wa kutoa maji kutoka Mto Bupigu.
Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (kushoto) akiwa ameambatana na Wahandisi wa RUWASA Mkoa wa Songwe wakielekea kwenye maeneo unapopita Mto Bupigu.
Wahandisi wa RUWASA Mkoa wa Songwe wakimuonyesha Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (wa pili kushoto) maeneo ya milima ambayo Mto Bupigu unatiririsha maji yake.
Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga alipotembelea Kijiji cha Bupigu kukagua mtiririko wa Mto Bupigu.
***
Na Mohammed Seif, Songwe
Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga amesema Serikali inatarajia kuwa na mradi mkubwa wa maji utakaohudumia miji mbalimbali katika Mkoa wa Songwe ili kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama.

Amesema hayo alipotembelea eneo la Mto Bupigu, kijiji cha Bupigu Wilayani Ileje Mkoa wa Songwe kwa dhamira ya kukagua vyanzo toshelevu vya maji katika miji yenye changamoto ya huduma ya maji.

“Katika milima hii ndipo kuna chanzo tunachokitarajia kuchukua maji takriban kilomita 75 kutoka Bupigu kuelekea mji wa Tunduma. Ni mradi ambao tunautengeneza yaani ‘project formulation’ ili tutafute fedha za kuanza rasmi kujenga mradi” Mhandisi Sanga alisema.

Alisema Serikali inatambua changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji kwa maeneo ya mijini mkoani humo na kwamba jitihada za makusudi zinaendelea kuchukuliwa ili kuwa na huduma toshelevu ya maji kwa wakazi wa miji hiyo.

“Kwa Mkoa huu wa Songwe, tunatambua changamoto kubwa ya maji ipo katika maeneo ya mijini, maeneo ya vijijini Serikali kupitia RUWASA imefanya kazi kubwa lakini mijini mathalan katika mji wa Tunduma mahitaji ni takriban lita milioni 17 kwa siku wakati maji yanayozalishwa ni chini ya lita milioni tano kwa siku” Mhandisi Sanga alisema.

Alisema Serikali imelenga kutoa maji Mto Bupigu na kuyafikisha katika mji wa Ileje ambapo ndipo chanzo kilipo, vijijini takriban 14 vipate maji kupitia mradi huo, makao makuu ya Mkoa wa Songwe yaani Vwawa, mji wa Tunduma, Mlowo na Mbozi.

Alifafanua kwamba matarajio ya Serikali ni kuhakikisha vyanzo toshelevu vya maji vinatumika kwa kuwa na miradi mikubwa ya maji ili kuwaondolea adha wananchi.

“Tunatarajia kutumia Mto Bupigu kujenga mradi mkubwa ambao utaondoa kabisa tatizo la maji katika mji wa Tunduma; ni ahadi ambayo tulikwishaitoa kupitia viongozi mbalimbali wakitaifa ambao wamefika huku” Mhandisi Sanga alibainisha.

Alisema katika ngazi ya Wizara ya Maji kufika kwake hapo ni kuashiria kwamba mradi huo sasa upo katika hatua za kutengeneza ili uweze kuanza na kuwaondolea wakazi wa Tunduma na miji mengine Mkoani humo changamoto ya upatikanaji wa maji.

No comments:

Powered by Blogger.