LIVE STREAM ADS

Header Ads

Zoezi la Usaili wa Makarani na Wasimamizi wa Sensa lakamilika Kongwa mkoani Dodoma

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma imekamilisha zoezi la usaili wa ajira za muda mfupi za makarani, wasimamizi wa maudhui na TEHAMA watakaohusika na zoezi la Sensa ya watu na MAKAZI itakalofanyika Agosti 23, 2022.

Akizungumza na Zabibu FM Radio, Julai 19, 2022 Mratibu wa Sensa wilayani Kongwa, Unambwe Erasto alisema zoezi hilo limefanyika katika kata zote 22 za Wilaya hiyo.

"Tunamshukuru Mungu zoezi limeenda salama katika maeneo yote, kama ambavyo tulitoa matangazo waombaji walijitokeza kwa nafasi walizoomba na kweli nitoe pongezi kwa wasimamizi wa zoezi hilo kwa namna ambavyo walihakikisha Kila kitu kinaenda sawa" alisema Unambwe.

Alisema kufanikiwa kwa zoezi hilo kunatokana na kamati ya Wilaya inayoongozwa na Mkuu wa Wilaya Mhe. Remidius Mwema kujipanga kikamilifu kwa kuutumia Mwongozo ambao ulitolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu na ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ambao uliwasaidia sana kuifanya hiyo kazi kuwa rahisi.

"Unajua Siku chache kabla ya kufanyika kwa zoezi hili ofisi ya Taifa ya Takwimu iliitoa Mwongozo wa namna ya kuendesha zoezi hili la usaili na kamati ya wilaya Siku mbili kabla ya zoezi hili tulitembelea katani na kutoa elimu ya namna ya kutumia Mwongozo huo" aliongeza Unambwe.

Aidha alisema baada ya usaili kukamilika matokeo yataidhinishwa na kamati ya Sensa ya Wilaya kwa hatua inayofata.

Akizungumzia changamoto zilizojitokeza, Unambwe alisema ni baadhi ya waombaji wa nafasi hizo (wasailiwa) kutokuja na nakala halisi za vyeti kama tangazo lilivyoelekeza.

Ikumbukwe kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilitangaza rasmi kuanza kupokea maombi ya kazi za muda za makarani na wasimamizi wa sensa ya watu na makazi kwa muda wa siku 14 kuanzia tarehe 05 Mei 2022 kupitia mfumo wa maombi ya kielektroniki.

Sensa ya Watu na Makazi hapa nchini inatarajiwa kufanyika tarehe 23, Agosti 2022 yenye kauli mbiu 'Sensa kwa Maendeleo, Jiandae Kuhesabiwa.
Wasimamizi wa Usaili wa Makarani na Wasimamizi wa Sensa Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma wakijadiliana jambo.
Na Maganga Gwensaga, Dodoma

No comments:

Powered by Blogger.