LIVE STREAM ADS

Header Ads

Mufti wa Tanzania kuongoza harambee ya ujenzi wa Vituo vya Afya Mwanza

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakari Zubery anatarajiwa kuongoza harambee ya ujenzi wa vituo saba vya Afya katika Wilaya za Mkoa wa Mwanza.

Hayo yameelezwa Julai 26, 2022 na Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Hassan Kabeke wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake na kuongeza kuwa harambee hiyo itafanyika Jumamosi Julai 30, 2022 katika uwanja wa Nyamagana Jijini Mwanza.

Sheikh Kabeke amesema harambee hiyo itahusisha makundi ya wananchi wote bila kujali dini ama kabila kwani jambo hilo ni la kijamii na kutumia fursa hiyo kuwaomba wadau mbalimbali kujitokeza kwa wingi kuchangia ujenzi huo.

Amesema siku hiyo watapokea mahitaji mbalimbali ikiwemo mchanga, kokoto, nondo, saruji na fedha ambazo zitasaidia kukamilisha ujenzi wa vituo hivyo.

"Nitumie nafasi hii kuwaomba wananchi wote walioko ndani na nje ya Mwanza kujitokeza kwa wingi kushiriki katika harambee yetu ili kwa pamoja tuweze kufanikisha zoezi hili la kujenga vituo vya afya katika Wilaya zote saba za Mkoa wetu wa Mwanza vitakavyowezesha kutoa huduma stahki kwa jamii" amesema Kabeke.
Sheikh Kabeke ameongeza kuwa maandalizi ya shughuli hiyo yamekamilika na baadhi ya viongozi wakiwemo wa dini na Serikali wamethibitisha kushiriki.

Kwa upande wake Mshauri Mkuu wa Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Swaleh Banyanga ameeleza jambo la afya ni la muhimu katika maisha ya mwanadamu hivyo kupitia harambee hiyo wananchi wajitolee kile walichonancho ili kuweza kusaidia kukamilisha ujenzi wa vituo hivyo vya afya.

"Faida kubwa ya kutoa ni kulinda mali ulizonazo na ni sadaka ambayo inatusaidia baada ya umauti hivyo ni wajibu wetu kutoa ili kuweka amana kwa Mwenyezi Mungu" amesema Banyanga.
Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Hassan Kabeke (wa nne) akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi mbalimbali wa dini.
Na Hellen Mtereko, Mwanza

No comments:

Powered by Blogger.