LIVE STREAM ADS

Header Ads

Wazazi wanaoruhusu watoto kufanya kazi za ndani waonywa

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Wazazi na walezi wenye watoto wanaosoma katika shule ya sekondari ya Ngomai iliyopo kata ya Ngomai wilayani Kongwa Mkoani Dodoma wametakiwa kuhakikisha wanawajengea msingi imara wa elimu kwani ndiyo ufunguo pekee wa maisha yao ya sasa na badae.

Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma, Remidius Mwema wakati akizungumza na wazazi pamoja na walezi wa wanafunzi wanaosoma katika shule ya sekondari Ngomai iliyopo kata ya Ngomai wakati wakati wa ziara yake katani hapo.

Amesema dhamira ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia katika kuhakikisha wanafunzi wanakuwa na mazingira rafiki ya kujisomea, imeondoa ada kuanzia elimu ya msingi mpaka kidato cha sita hivyo lazima kila mmoja awe na uchungu na mtoto wake ahakikishe anafanya bidii katika kuhakikisha anapata elimu.

“Suala la elimu ni suala la msingi sana hivyo ni lazima kila mmoja ahakikishe anafanya kwa sehemu yake, maafisa wa elimu kata, vijiji na wilaya pamoja na jamii nzima kila mmoja aguswe na suala la elimu tunahitaji kufanya vizuri" alisema Mkuu wa Wilaya

Amesema Serikali inaweza kuweka mazingira mazuri kwa wanafunzi lakini kama hakuna utayari wa mwanafunzi wenyewe wa ufauli, watapata wakati mgumu sana na hawatoweza kupata ufaulu mzuri hivyo jambo la msingi wanafunzi waone thamani kubwa ya kuweza kufanya vizuri kwenye masomo.
Ameongeza kuwa wilaya ya kongwa imekuwa ikifanya vibaya kielimu ukiringanisha na wilaya zingine zilizopo Mkoani Dodoma , hivyo basi Wazazi, walezi na wasimamizi wa elimu wanatakiwa kuhakikisha kila mmoja anafanya sehemu yake.

"Na ndio maana kila siku nafatilia hata hawa walimu, nawaomba viongozi wote wa serikali kuanzia kata na vijiji wote tufahamu jukumu letu la msingi , niwaombe wakuu wangu wa idara na wataalam wote na jamii yote lazima kila mtu atimize wajibu wake" aliongeza.

Sambamba na hilo Mkuu huyo wa Wilaya amekea tabia ya baadhi ya wazazi na walezi wa kata hiyo kuwapeleka watoto wao mijini kufanya kazi za ndani akisema kufanya hivyo ni kosa na Serikali ya wilaya haitosita kuwachukulia hatua kali wazazi wote wenye tabia hiyo na kuwataka wazazi wote waliopeleka watoto wao mjini kuwarudisha haraka shuleni.

Mbali na hilo amekemea tabia ya utoro katika shule hiyo na kumwelekeza Mkuu huyo wa shule kumpelekea orodha ya majina ya watoto watoro na majina ya wazazi au walezi wa watoto wanaosoma shuleni hapo ili hatua mbalimbali ziweze kuchukuliwa.

Akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara mkuu huyo wa Wilaya ameelezea mafanikio ya serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuanzia elimu, afya na miundombinu pamoja na uwepo wa zoezi la sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika tarehe 23 mwezi wa nane mwaka huu.
Amesema zoezi la sensa ni muhimu sana kwani kupitia sensa serikali inaweza kufanya maendeleo kwa wananchi kupitia taarifa sahihi zinazokusanywa hivyo basi ni vyema kila mmoja aweze kutoa ushirikiano kujitokeza kuhesabia.

"Ndugu zangu sensa ni ya muhimu sana kwani ni maendeleo, ni elimu, ni barabara, ni afya , ni umeme na tunasema haya ili mjue, leo mnasema mkuu wa wilaya tunataka barabara, kituo cha polisi, nyumba za watumishi, kituo cha afya nk, tunapofahamu idadi ya watu maana yake tunaona kwamba kuna uhitaji wa jambo hilo katika eneo husika" alisema

Ameongeza kuwa Serikali ya awamu ya sita imefanya mambo makubwa sana wilayani Kongwa kwa kutoa fedha za ujenzi wa vituo vya afya Sejeli, Chitego, Pandambili, Mkoka, Songambele, Chamkoroma na maeneo mengine pamoja na ujenzi wa madarasa, kwahiyo sensa inasaidia kwenye mipango ya Serikali kuleta maendeleo.

Katika ziara hiyo Mkuu huyo aliambatana na wakuu wa idara mbalimbali wakiwemo Nida, Tanesco, Tarura, Ruwasa pamoja na maafisa wa ardhi ambao walijibu kero mbalimbali za wananchi.
Na Maganga Gwensaga, Dodoma

No comments:

Powered by Blogger.