LIVE STREAM ADS

Header Ads

Kampeni ya kuchangia Damu Salama yaleta matokeo chanya

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Mratibu wa Kampeni ya Uhamasishaji wa kuchangia damu kwa hiari Amos John maarufu MC MZUNGU MWEUSI amewashukuru wananchi walioshiriki kampeni hiyo iliyokwenda sanjari na kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu Sensa ya Watu na Makazi Agosti 23,2022 huku akiiomba jamii kuendelea kujitokeza kuchangia damu ili kuokoa maisha ya wengine.

Aliyasema hayo Jumamosi Julai 02, 2022 wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya wananchi kushiriki zoezi la kuchangia damu kwa hiari ambalo limefanyika kwenye uwanja wa CCM Kambarage mjini Shinyanga.

Amos John ambaye ni Mwandishi wa Habari na mtangazaji wa Radio Kwizera Fm Mkoa wa Shinyanga aliwasisitiza wananchi kuendelea kuunga mkono shughuli za uchangiaji damu ili kuokoa maisha ya watu wenye uhitaji wakiwemo wajawazito, watoto na wahanga wa ajali.

Alisema aliguswa na kuamua kuandaa Kampeni ya damu salama kwa lengo la kuhamasisha jamii kujenga utaratibu wa kuchangia damu ambapo ameshirikiana na kitengo cha damu salama Manispaa ya Shinyanga.

"Niliguswa na kuamua kushirikiana na kitengo cha damu salama Manispaa ya Shinyanga kuandaa kampeni ya damu salama kwa lengo moja tu la kuhakikisha tunahamasisha wananchi kujenga utamaduni kuchangia damu ili waweze kuokoa maisha ya ndugu zetu wenye uhitaji wa damu" alisema Amos.

Naye Mratibu wa Huduma za Maabara Manispaa ya Shinyanga, Saumu Ibrahim alisema kampeni hiyo imekuwa na mafanikio kwani wananchi wamejitokeza kuchangia damu.

"Tunamshukuru Mungu kwa leo tumeweza kupata UNIT zaidi ya 14 na mahitaji yetu kwa Manispaa kwa siku tunahitaji kutumia UNIT 9 tunaimani kwamba tumepata kitu cha kuweza kuwasaidia watu wenye uhitaji, wito wangu kwa wananchi wa Shinyanga wajitokeze kuchangia damu" alisema Ibrahim na kuongeza;

"Suala la damu kila mtu ni mhitaji wa damu mtarajiwa ukipata mgonjwa mwenye shida ya damu au ukipata shida ya damu ndiyo utajua umuhimu wa kuchangia damu na suala la damu limekuwa ni changamoto mno kwahiyo uhitaji wa damu ni mkubwa niwaombe sana watanzania kwa ujumla tuguswe kwa kuona umuhimu wa kuchangia damu" alisema Ibrahim.

Baadhi ya wakazi mkoani Shinyanga ambao walishiriki zoezi kampeni hiyo wameeleza kuwa wamehamasika katika zoezi la uchangiaji damu kwa lengo la kusaidia watu wenye uhitaji huku wakitoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa ajili ya kuchangia damu ili kuwasaidia wahitaji.

Aidha wananchi hao waliwashukuru waandaaji wa kampeni hiyo ya kuchangia damu ambapo wamesema itasaidia kuondoa changamoto ya upungufu wa damu salama.
MC Mzungu Mweusi akielezea kuhusu Kampeni ya Uchangiaji damu salama.
Wananchi wakiendelea kuchangia damu.
Na Mapuli Misalaba, Shinyanga

No comments:

Powered by Blogger.