LIVE STREAM ADS

Header Ads

Dodoma: Kamati ya Usaili wa ajira za Sensa yatakiwa kuzingatia Mwongozo

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Kamati ya Sensa ya Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma, imelitaka jopo la usaili wa makarani na wasimamizi wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 kufuata kikamilifu mwongozo uliotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali wakati wa kuwafanyia usahili waombaji wa nafasi za ajira za muda wa zoezi la Sensa.

Kamati hiyo inayoongozwa na Mwenyekiti wake Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Remidius Mwema imetoa agizo hilo Julai 16, 2022 kupitia Mratibu wa Sensa wa Wilaya Unambwe Erasto wakati akizungumza na wajumbe watakaounda jopo hilo kutoka Mata za Mlali na Kibaigwa katika kikao kazi cha kupitia mwongozo wa uchambuzi wa maombi ya ajira za muda. 

Alisema malengo ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha zoezi hili linafanikiwa hivyo lazima wasimamizi na makarani ambao watasimamia zoezi hilo lazima wapatikane kupitia kwenye mchakato huo. 

Aidha alisema ili zoezi hilo liweze kuleta ni lazima watendaji wa zoezi hilo wawe wenye weledi wa kutosha ambao watasimamia na kulifanya zoezi hili kwa uzalendo mkubwa hivyo wao kama jopo la usaili ni vyema wakatumia mwongozo uliotolewa ili kuwapata watu sahihi. 

"Zoezi hili ni la kizalendo, najua miongoni mwenu mna watu ambao mnafahamiana na inawezekana wameomba nafasi mbalimbali, nyie mtakaopata nafasi ya kuwepo kwenye hilo jopo la kusimamia usaili nawaomba mfuate miongozo inavyosema" alisema Enambwe 
Mratibu wa Sensa Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma, Unambwe Erasto.


Aliwataka viongozi hao kutochagua mtu kwa kumfahamu, udugu, urafiki au mahusiano yoyote yale kwani mwongozo upo wazi ukieleza sifa na vigezo vya mwombaji kwa nafasi husika. 

"Naomba sana tuangalie mwongozo unasema nini kwa kila nafasi, na niwaambie tu kamati iko makini sana hatutakubali udanganyifu wa aina yoyote na zaidi muwe watu wenye kutunza siri na hasa kama utapata nafasi ya kuingia kwenye hilo jopo, kwani Serikali haitosita kumchukulia hatua mjumbe yoyote ambaye atakwenda kinyume na taratibu zilizowekwa" aliongeza Mratibu.

Kwa upande wao wajumbe wa jopo hilo kutoka katika kata hizo walimhakkishia Mratibu wa Sensa wa Wilaya Kongwa kuwa watazingatia mwongozo waliopewa na watasimamia maelekezo yote yaliyotolewa katika kuhakikisha zoezi hilo linakwenda kama lilivyokusudiwa. 

Ikumbukwe Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilitangaza rasmi kuanza kupokea maombi ya kazi za muda za makarani na wasimamizi wa sensa ya watu na makazi kwa muda wa siku 14 kuanzia tarehe 5 Mei 2022 kupitia mfumo wa maombi ya kielektroniki.

Hadi kufikia tarehe 19 Mei, 2022 saa 6:00 usiku jumla ya maombi 689, 935 ya kazi za muda za makarani na wasimamizi yalikuwa yamepokelewa ikilinganishwa na nafasi 205,000 zinazohitajika kujazwa. 

Sensa ya watu na makazi hapa nchini inatarajiwa kufanyika tarehe 23, Agosti mwaka 2022 yenye kauli mbiu "Sensa kwa Maendeleo, Jiandae Kuhesabiwa".
Na Maganga Gensaga, Dodoma

No comments:

Powered by Blogger.