LIVE STREAM ADS

Header Ads

Mabroka watakiwa kupambana na utoroshaji madini

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel (kulia) ametoa rai kwa Chama cha Mabroka wa Madini nchini (CHAMMATA) kuthibiti wafanyabiashara wenye tabia ya kutorosha madini ili kuimarisha ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali.

Mhandisi Gabriel alitoa rai hiyo Julai 13, 2022 wakati akizungumza kwenye Mkutano wa Halmashauri Kuu ya CHAMMATA uliofanyika jijini Mwanza akimwakilisha Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko.

Aidha Mhandisi Gabriel aliipongeza CHAMMATA kwa kupata usajili na kuahidi kuwa Seriikali kupitia Wizara ya Madini itaendelea kushirikiana na chama hicho ikiwa ni pamoja na kufanikisha suala la kufanya biashara za madini kwa kutumia leseni ya aina moja kokote nchini.

Naye Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Emily Kasagala akimwakilisha Katibu Tawala Mkoa Mwanza, Ngusa Samike aliipongeza CHAMMATA kwa umoja wao na kuwaalika kushiriki Maonesho ya Kilimo, Mifugo na Biashara Kanda ya Ziwa Magharibi yatakayofanyika viwanja vya Nyamhongolo kuanzia Agosti 01 hadi 08, 2022.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CHAMMATA, Jeremia Simon aliishukuru Serikali kupitia Wizara ya Madini kwa kuanzisha mfumo wa masoko rasmi ya madini ambayo yameleta maendeleo makubwa kutokana na kuondokana na biashara holela ya madini huku pia wakiacha kutembea na fedha nyingi hali iliyokua inahatarisha usalama wao. 

"Mfanyabiashara yeyote wa madini atakayetorosha madini CHAMMATA itachukua hatua kali kwake ikiwa ni pamoja na kuishauri Tume ya Madini kumnyang'anya leseni na kuhakikisha hafanyi tena biashara ya Madini nchini" alionya Simon akiunga mkono kauli ya RC Mwanza.

Aliongeza kuwa lengo la kuanzishwa Chama cha Mabroka wa Madini Tanzania (CHAMMATA) ni kuwa na daraja la kuwaunganisha wafanyabiashara wa madini na Serikali kupitia taasisi zake kama Tume ya Madini, kutetea na kusimamia haki za wafanyabiashara wa madini, vito na chuma.
Afisa Madini Mkazi Mkoa Mwanza, Mhandisi Nyaisara Mgaya (pichani) alisema mabroka ni daraja la kuunganisha wachimbaji wa madini na wauzaji wakubwa, hivyo ni watu muhimu wa kushirikiana na Tume ya Madini katika kupambana na utoroshaji madini.
Na Steven Nyamiti, WM

No comments:

Powered by Blogger.