LIVE STREAM ADS

Header Ads

Wafanyakazi TANESCO watakiwa kujiamini

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Waziri wa Nishati, January Makamba amewataka wafanyakazi wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO), kujiamini na kufanyakazi kwa weledi ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora.

Waziri Makamba ameyasema hayo Julai 14, 2022 wakati akizungumza na wafanyakazi na menejimenti ya TANESCO Mkoa Mwanza.

Amesema wafanyakazi wa Shirika hilo wanapaswa kutimiza wajimu wao kwa weledi huku wakiwa wawazi kwa watenda hatua itakayosaidia kuondoa malalamiko ambayo hujitokeza wananchi wanapokosa huduma ya umeme.
Makamba amesema lengo la Serikali ni kuweka mazingira bora kwa wafanyakazi kutimiza majukumu yao bila hofu na hata wanaposhindwa kufikia malengo wasaidiwe kuyafikia na si kuwaza kuwafukuza.

"Naamini mfanyakazi mwenye weledi hawezi kukata umeme makusudi kama ilivyokuwa inaelezwa awali huko mitaani kwamba kuna hujuma, ndiyo maana hamkuona tunajitokeza kumtafuta mchawi nani wakati umeme unakatika mara kwa mara kutokana na sababu ambazo mlizishughulikia" amesema Makamba.

Katika hatua nyingine Waziri Makamba amewapongeza wafanyakazi wa TANESCO Mkoa Mwanza kwa kuibuka kidedea katika kuhamasisha wananchi kutumia huduma ya Kidigitali ya 'Nikonect' inayomwezesha mteja kupata kwa wakati huduma mbalimbali ikiwemo kuunganishiwa umeme.
Meneja wa TANESCO Mkoa Mwanza, Mhandisi Said Msemo amesema hali ya upatikaji wa umeme mkoani Mwanza imeimarika na kwamba Shirika hilo linaendelea na jitihada za kufikisha nishati hiyo kwa wateja wapya akisema kiasi cha shilingi bilioni 16 kilichotengwa na Serikali kitasaidia kuimarisha upatikanaji wa umeme mkoani Mwanza.
Na George Binagi-GB Pazzo, BMG

No comments:

Powered by Blogger.