LIVE STREAM ADS

Header Ads

Mgao wa maji watikisa machinjio ya ng'ombe Mwanza

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Wafanyabiashara na wafanyakazi (wachinjaji) katika machinjio ya ng'ombe Igoma jijini Mwanza wamelia na mgao wa maji uliowakumba wakisema umesababisha wafanye kazi katika mazingira magumu na yasiyo rafiki kiafya.

Wameyasema hayo alfajili ya Jumatatu Julai 11, 2022 wakati wa ziara ya Mstahiki Meya wa Jiji la Mwanza, Sima Constantine iliyolenga kukagua shughuli mbalimbali kwenye machinjio hiyo.

Francis Kenyunku ambaye ni mfanyabiashara wa nyama na pia mchinjaji kwenye machinjio hiyo, amesema ukosefu wa maji umesababisha changamoto kubwa ikiwemo uoshaji wa nyama/ utumbo, kufanya usafi kwenye vizimba vya kuchinjia pamoja na wafanyakazi kunawa baada ya shughuli ya kuchinja.

"Kwa muda wa wiki tatu sasa hatuna maji, watu wanalazimika kuja na maji kutoka majumbani kwa ajili ya kuosha utumbo hivyo tunaiomba Serikali iweze kututatulia changamoto hii ili tuweze kufanya kazi katika mazingira rafiki" amesema Kenyunku.

Kwa upande wake Kalaba Kesi ambaye pia ni mfanyabiashara katika machinjio hiyo amesema licha ya kuwepo changamoto ya maji, bado machinjio hiyo haina utaratibu wa watu kuingia kwani wamekuwa wakiingia bila mpangilio na hivyo kuomba kujengwa uzio hatua itakayosaidia kuondoa adha iliyopo sasa.

Ameongeza kuwa miundombinu ya kuingia machinjioni ni mibovu, sehemu ya kushushia mifugo siyo rafiki hatua inayohatarisha mifugo kuvunjika miguu

Mstahiki Meya wa Jiji la Mwanza, Sima Constantine amesema maji ni ya muhimu katika uendeshaji wa shughuli mbalimbali kwenye machinjio hiyo na hivyo kuahidi kufanya mazungmzo na uongozi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (MWAUWASA) ili kupata ufumbuzi wa changamoto ya maji.

Kuhusu suala la ujenzi wa uzio katika machinjio hiyo, Sima ameahidi kulifanyia kazi kwa kulifikisha katika vikao vya maamuzi ili kuhakikisha Halmashauri ya Jiji la Mwanza inaliweka kwenye mipango ya utekelezaji.

Akizungumza na BMG, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano MWAUWASA, Mohamed Seif amekiri kuwepo changamoto ya uhaba wa maji katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Mwanza hususani maeneo ya pembezoni kutokana na hitilafu ya kuungua mota mbili za kuendesha mitambo ya kuzalisha na kusukuma maji.

Seif amesema hatua mbalimbali zimechukuliwa ili kukabiliana na uhaba huo ikiwa ni pamoja na kubadili ratiba za mgao wa maji kuhakikisha maeneo yote yanafikiwa na huduma hiyo kwa siku tofauti tofauti na kwamba tayari MWAUWASA imeagiza mota mpya ambazo zinatarajiwa kuwasili katika kipindi cha wiki mbili zijazo.

"Tunawaomba radhi wateja wetu kwa usumbufu wanaopitia, tunawasihi kuhifadhi maji kila yanapowafikia na pia tuendelee kuwasiliana kwa changamoto zinazojitokeza ili kuzipatia ufumbuzi mapema iwezekanavyo" ameomba Seif.
Na Hellen Mtereko , Mwanza
Mstahiki Meya wa Jiji la Mwanza, Sima Constantine akikagua mazingira ya kutundikia nyama katika machinjio ya ng'ombe Igoma.
Mstahiki Meya wa Jiji la Mwanza, Sima Constantine (katikati) akizungumza na wafanyakazi na wafanyabiashara wa nyama katika machinjio ya ng'ombe Igoma.

No comments:

Powered by Blogger.